Makala

TAHARIRI: Ushuru utawaumiza wananchi wanyonge

September 3rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

KUANZIA Jumapili, Wakenya wameanza kukabiliwa na ushuru mpya wa asilimia 16 unaotozwa mafuta. Ushuru huo unaambatana na Sheria ya Fedha ya 2013 ambayo ilirefusha kipindi cha kuanza kutekelezwa kwa sheria kwa miaka mitatu na kucheleweshwa tena kwa miaka mingine miwili.

Ushuru huo ulianza kutekelezwa na kupandisha bei ya mafuta ya petroli, dizeli na yale ya taa. Hayo ni kinyume na matarajio ya wananchi, hasa baada ya Bunge wiki jana kufanyia marekebisho sheria hiyo na kuahirisha kwa miaka mingine miwili.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed aliwasilisha mswada uliopitishwa ili kuahirisha utekelezaji wa sheria hiyo kwa miaka miwili kwa lengo la kuwakinga wananchi. Hata hivyo, mswada huo haukutiwa sahihi na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kuelekea Uchina kwa mkutano, hali ambayo ilitoa nafasi kwa KRA kutekeleza sheria hiyo.

Ushuru huo unatekelezwa wakati ambapo imebainika kuwa kuna ushuru mwingine unaotozwa dawa za kuua wadudu zinazotumiwa na wakulima.

Kuongeza ushuru huu bila shaka kutakuwa na athari ya moja kwa moja kwa mwananchi. Kwanza, wamiliki wa magari ya usafiri wa umma wanasema wamechoshwa na kupanda kila siku kwa mafuta, na wanapanga kupandisha nauli.

Iwapo wenye viwanda nao watahisi mzigo katika gharama ya utengenezaji bidhaa, bei ya chakula na bidhaa nyingine za matumizi itapanda. Kwa kuwa mafuta hutegemewa katika shughuli nyingi za uchumi wa Kenya, kuna uwezekano mkubwa kuwa bei za bidhaa muhimu zitapanda maradufu.

Mafuta hayafai kuuzwa kwa bei ya juu Kenya kushinda mataifa jirani kama vile Ethiopia, ambayo hata hayana bandari. Kenya haiko mbali na Saudi Arania na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati, na inaweza kununua mafuta kwa bei rahisi na kuyaptitisha kwa bomba kupitia Moyale.

Ushuru mpya kwa dawa za kuua wadudu mashambani bila shaka utakuwa na athari katika ukuzaji chakula cha kutosha. Hili ni kinyume na mipango ya serikali katika mojawapo ya nguzu kuu nne.

Serikali imetangaza wazi kuwa mojawapo ya mambo ambayo Rais Kenyatta angependa kukumbukwa nayo ni kuhakikisha Wakenya wana chakula cha kutosha.

Nguzo hii kuu inaweza kutekelezwa kwa kuwepo mbinu bora na mazingira mazuri ya kuzalisha chakula kwa wingi. Je, hili litawezekana vipi ikiwa mkulima analimbikiziwa mzigo wa ushuru?