HabariSiasa

BEI GHALI: Omtatah afika mahakamani kuokoa Wakenya

September 3rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah Jumatatu aliishtaki Serikali kwa kuongeza ushuru wa thamani ya ziada (VAT) kwa asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta akisema umekandamiza haki za kiuchumi za Wakenya.

Katika kesi ya dharura aliyowasilisha katika mahakama kuu, Bw Omtatah alisema nyongeza hiyo imesababisha kuongezwa kwa bei za mafuta ya Petroli, Dizeli na mafuta taa.

Mwanaharakati huyu amesema nyongeza hii ya ushuru huu wa VAT imesababisha kuongezwa kwa nauli ya magari ya usafiri wa umma.

Mahakama imeelezwa nyongeza hii imesababisha mtafaruku kote nchini na akaomba maagizo yatolewe yakifutilia mbali nyongeza hii ya asili mia 16.

Bw Omtatah amemshtaki Waziri wa Fedha, Henry Rotich, Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) na Mwanasheria Mkuu (AG).

Ushahidi aliowasilisha mahakamani ni kwamba nyongeza hiyo ya VAT ya Septemba 1 2018 ni ukiukaji wa katiba.

“Kuongeza ushuru huu wa VAT kwa bidhaa za mafuta kwa asilimia 16 kuna athari kubwa kwa mwananchi,” alisema katika afidaviti aliyowasilisha kortini.

Bw Omtatah ameomba mahakama isitishe kutekelezwa kwa ushuru huo kwa vile unaathiri sekta zote za uchumi.

Bw Omtatah amesema usalama wa kitaifa umetishika kwa vile nyongeza ya ushuru huu inasukumwa na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kinyume cha Kifungu nambari 238 cha Katiba.

Amedokeza kuwa IMF ndiyo imesukuma nyongeza hii ya asili miaka 16 ya ushuru wa VAT kwa lengo la kumkandamiza mlipaushuru.

Amesema bado Rais Uhuru Kenyatta hajaidhinisha Hoja ya Fedha  ya 2018 ambayo imepingwa na bunge na wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi.

Bunge lilisema utekelezwaji wa hoja hiyo uahirishwe kwa vile uko na athari mbaya kiuchumi na utasababisha kuongezwa kwa gharama za huduma na bidhaa muhimu na gharama ya maisha kupanda.

Bw Omtatah amesema kuwa nyongeza hii itapelekea kuongezwa kwa ushuru unaotozwa uimarishaji wa bidhaa za mafuta, ushuru wa kuthibiti bidhaa hizi, ushuru wa uchukuzi kwa reli miongoni mwa nyingine.

Mwanaharakati huyo amesema asilimia 60 ya Wakenya hutegemea bidhaa za mafuta kwa kuendeleza shughuli viwandani na hata uchukuzi.

Nyongeza hii imesababishwa kuongezwa mara moja kwa nauli na bidhaa nyinginezo zinazohitajika kwa matumizi ya kila siku nyumbani. Alisema abiria wataumizwa na nyongeza.

“Gharama ya uzalishaji bidhaa viwandani itaongezeka mara moja na hii iko na maana kwamba ukusanyaji wa ushuru na KRA utaathirika pakubwa kwa vile walipa ushuru wamesongwa na nyongeza hii,” asema Bw Omtatah.

“Hatuwezi kujadilia kukua kwa uchumi na huku tunaongeza ushuru wa mafuta ya petroli na kuongeza gharama ya uzalishaji bidhaa,” amesema Bw Omtatah

Mnamo Alhamisi wiki iliyopita bunge lilifanyia marekebisho mswada wa Fedha wa 2018 na kuamuru nyongeza hiyo ya ushuru wa VAT uanze kutekelezwa Septemba  1 2020.

Bw Rotich ameanza kutekeleza hoja hii ilhali Rais Kenyatta hajaitia saini.

Kesi hiyo itasikizwa Jumanne.