• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Harambe Stars kujaribu kuiuma Ghana bila Wanyama

Harambe Stars kujaribu kuiuma Ghana bila Wanyama

Na Geoffrey Anene

SASA ni rasmi Harambee Stars ya Kenya itaingia katika vita vya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 dhidi ya Black Stars ya Ghana bila nyota Victor Wanyama hapo Septemba 8, 2018.

Kiungo wa Tottenham Hotspur, Wanyama, ambaye ni nahodha wa Kenya, hajapona jeraha la goti. Alijeruhiwa katika klabu yake kabla ya Ligi Kuu ya Uingereza ya msimu 2018-2019 kuanza mwezi mmoja uliopita (Agosti 10).

Beki matata David ‘Calabar’ Owino, ambaye anatarajiwa kutwikwa majukumu ya unahodha, pia yumo hatarini kukosa mchuano huu wa Kenya wa pili katika Kundi F.

“Owino amekuwa na tatizo asubuhi hii, jeraha dogo la mguu na atafanyiwa uchunguzi katika kipindi cha pili cha mazoezi baadaye leo (Jumatano),” Kocha Sebastien Migne amesema, huku akikiri kukosekana kwa Wanyama ni pigo kubwa. Ameongeza kwamba “hawezi kulia” kuhusu ukosefu wa huduma za Wanyama, bali kutafuta suluhu.

Mfaransa huyu amekiri kwamba Ghana ni mpinzani mkali. “Ghana ni timu kali. Ni mojawapo ya timu nzuri duniani. Si siri ni kibarua kigumu kuchapa Ghana, lakini katika soka chochote chawezekana,” Migne amesema na kuongeza hana tumbo joto, ingawa ana presha kidogo na anatumai vijana wake watajituma vilivyo kuweka tabasamu katika nyuso za Wakenya. Ameomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani utakaoandaa mchuano huu muhimu kuanzia saa kumi jioni Jumamosi.

Migne amefichua kwamba kipa bora wa Kenya na Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mwaka 2017, Patrick Matasi ndiye chaguo lake nambari moja michumani.

Bonface Oluch wa Gor Mahia, ambaye amekuwa kipa nambari moja wa Kenya, hata hayumo kikosini kabisa. Ian Otieno (Red Arrows, Zambia) na Farouk Shikalo (Bandari) ni makipa wengine Migne atategemea Matasi akipata tatizo ama akifanya masihara.

Mvamizi Michael Olunga, ambaye ni mchezaji wa Harambee Stars aliye an rekodi nzuri mbele ya lango wakati huu, amesema ni fahari kubwa kujumuishwa kikosini kwa majukumu ya timu ya taifa. Ameongeza kwamba wachezaji wanasubiri mchuano huu kwa hamu kubwa. “Tunafahamu Ghana ni timu kali, lakini tunalenga kujitolea kwa dhati kupata matokeo mazuri.

Kwa bahati mbaya, tulipoteza mechi yetu ya ufunguzi dhidi ya Sierra Leone (2-1), lakini nguvu zetu zote na akili zetu ziko katika mechi hii dhidi ya Ghana. Tutajiweka mahali pazuri tukipata matokeo mema dhidi ya Ghana,” amesema Olunga, ambaye alijiunga na Kashiwa Reysol kwenye Ligi Kuu ya Japan mnamo Agosti 10, 2018 kutoka Guizhou Hengfeng nchini Uchina.

Owino, ambaye husakata soka yake ya malipo katika klabu ya Zesco nchini Zambia, anaamini wenyeji Kenya wamejiandaa vyema tayari kupata matokeo mazuri. “Itakuwa mechi ngumu kwa sababu Ghana ni timu yenye uzoefu mkubwa katika mashindano makubwa.

Hata hivyo, najua tukiweka akili zetu zote na mitazamo yetu katika mchuano huu tutapata matokeo mazuri. Naomba mashabiki wajitokeze kwa wingi. Hatutawasikitisha,” Owino amesema Jumatano baada ya kipindi cha mazoezi cha asubuhi katika uwanja wa KSMS mtaani Ruaraka jijini Nairobi.

Ghana imekuwa ikipiga kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia Septemba 3 na inatarajiwa jijini Nairobi wakati wowote.

Tiketi za mechi hii ni Sh200 (kawaida) na Sh1,000 (VIP).

Janny Sikazwe atakuwa refa wa kupuliza kipenga katika mchuano huu akisaidiwa na raia wenzake kutoka Zambia Oliver Gift Mweene na Kabwe Chansa, huku Wisdom Chewe akiwa afisa wanne. Jean-Albert Rollin kutoka Reunion ni kamishna wa mechi.

Ghana inaongoza Kundi F kwa alama tatu baada ya kulipua Ethiopia 5-0 mjini Kumasi. Sierra Leone pia ina idadi sawa za alama, lakini inashikilia nafasi ya pili kutokana na tofauti ya ubora wa magoli. Ilizaba Kenya 2-1 jijini Freetown katika mechi ambayo Olunga alifunga bao la kufutia machozi.

Kenya haijawahi kuingia AFCON tangu ishiriki makala ya mwaka 2004 nchini Tunisia.

Baada ya kulimana na Ghana hapo Jumamosi, Kenya itapimana nguvu na Malawi mnamo Septemba 11 uwanjani Kasarani. Itamenyana na Ethiopia ugenini Oktoba 10 na kisha nyumbani Oktoba 14 katika mechi zingine za Kundi F kabla ya kufunga mwaka dhidi ya Sierra Leone jijini Nairobi mnamo Novemba 18. Mechi ya mwisho ya vijana wa Migne katika kampeni ya kuingia AFCON mwaka 2019 itakuwa dhidi ya Ghana hapo Machi 22, 2019 ugenini.

Kikosi cha Kenya:

Makipa – Patrick Matasi (Tusker), Farouk Shikalo (Bandari) na Ian Otieno (Red Arrows, Zambia);

Mabeki – Philemon Otieno (Gor Mahia), Jockins Atudo (Posta Rangers), Dennis Odhiambo (Sofapaka), Joash Onyango (Gor Mahia) Benard Ochieng (Vihiga United), Abud Omar (Cercle Brugge, Ubelgiji), David Ochieng’ (Brommapojkarna, Uswidi), Eric Ouma (Vasalund, Uswidi), Joseph Okumu (AFC Ann Arbor, Marekani), Musa Mohammed (Nkana, Zambia) na David Owino (Zesco United, Zambia);

Viungo – Francis Kahata (Gor Mahia), Abdallah Hassan (Bandari), Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), Eric Johanna (Brommapojkarna, Uswidi), Ismail Gonzalez (Las Palmas Atletico, Uhispania) na Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji);

Washambuliaji – Piston Mutamba (Sofapaka), Jesse Were (Zesco United, Zambia), Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan) na Ovella Ochieng (Vasalund, Uswidi).

You can share this post!

Mahakama yasitisha ushuru wa 16% kwa muda

Rwanda kukosa huduma za Tuyisenge AFCON

adminleo