• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
Mwanafunzi aitishwa mbuzi kwa kula nyama ya wenzake

Mwanafunzi aitishwa mbuzi kwa kula nyama ya wenzake

STEPHEN MUNYIRI na PETER MBURU

SHULE moja ya Upili inamulikwa kwa kutoa adhabu isiyo ya kawaida kwa wanafunzi, baada ya kumshurutisha mwanafunzi wa kidato cha nne aliyetuhumiwa kula mlo wa nyama wa wanafunzi wengine kununua mbuzi mzima.

Iliwabidi wazazi wa mwanafunzi huyo wa Shule ya Upili ya Kanjuri, Kaunti ya Nyeri kulipa mwalimu mkuu Sh8,000 za kununua mbuzi, ili mwanao anayetarajia kufanya mtihani wa kitaifa mwaka huu kuruhusiwa kurejea darasani baada ya kutimuliwa.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kula nyama iliyotengwa kuwa ya wenzake waliofuzu muhula uliopita, akiwa pamoja na wengine ambao hawakutambulika.

Kulingana na barua iliyoandikiwa wazazi wa mwanafunzi huyo na mwalimu mkuu Bw J.K Karanja, mwanafunzi huyo alikuwa na makossa manne ya utovu wa nidhamu yakiwemo kula nyama ya wanafunzi wenzake.

Aidha, alituhumiwa kula minofu hiyo pamoja na wenzake na kuingiza na kuuzia wanafunzi wenzake peremende kwenye bweni.

“Yafuatayo yanafaa kutimizwa ili akubaliwe kurejea shuleni, alipe gharama ya kununua mbuzi mwingine, kumchinja na kupima nyama yake- Sh8,000,” ikasema barua iliyofikishiwa wazazi.

Mamake mwanafunzi huyo alilalamika kuwa hatua ya shule haikuwa njema, akisema alilipa pesa hizo ili tu mwanaye asiadhiriwe kimasomo.

“Ni mwanafunzi wa kidato cha nne na sikutaka akose kuhudhuria masomo, lakini naamini hii ni hadithi isiyo ya kweli,” Bi Margaret Wamaitha akasema.

Mwalimu mkuu naye alikiri kuwa shule ilifanya hivyo, akisema kuwa wizara ya elimu ilikuwa na ufahamu wa hatua hiyo.

“Kesi hiyo ilisuluhishwa kwa utulivu na mwanafunzi ameruhusiwa kurejea shuleni,” Bw Karanja akasema.

You can share this post!

Ajabu ya klabu kuuza wachezaji wote 18 na kununua mbuzi 10

Shule ya Padre yafungwa kwa dhuluma za kimapenzi na...

adminleo