LAMU: Wakazi zaidi ya 2,000 walia njaa
NA KALUME KAZUNGU
ZAIDI ya wakazi 2000 wa jamii ya Waboni wanoishi kwenye Wadi ya Basuba, Kaunti ya Lamu wanakabiliwa na njaa kufuatia mazao yao kuharibiwa na wadudu na mvua kubwa iliyoshuhudiwa eneo hilo mwaka huu.
Wakazi sasa wamelazimika kurejelea maisha ya kuchuma matunda ya mwituni ili kukimu familia zao.
Mzee wa Nyumba Kumi eneo la Basuba, Noya Buli, aliambia wanahabari Alhamisi kwamba ukosefu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab pia umepelekea kukosekana kwa bidhaa kwani magari yaliyokuwa yakisambaza bidhaa hizo, ikiwemo vyakula Basuba yalikatiza mpango huo.
Kulingana na Bw Buli, mashirika yasiyo ya kiserikali pia yalikatiza mpango uliokuwa ukiendelea wa kuwasambazia Waboni misaada Basuba kutokana na kukosekana kwa njia za kusafirishia misaada hiyo.
Utafiti uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa idadi kubwa ya watoto eneo hilo wako kwenye hatari ya kuugua utapiamlo kufuatia ukosefu wa lishe bora unaochangiwa na umaskini uliokithiri miongoni mwa familia nyingi.
“Hatujavuna chochote mashambani mwaka huu kutokana na wadudu waliovamia na kuharibu mimea yetu. Isitoshe, mvua kubwa iliyonyesha mwaka huu pia iliharibu mimea mashambani. Njaa imetuzonga na tunalazimika kutafuta matunda ya msituni ili kukimu familia zetu. Hayo matunda pia yamevamiwa na wadudu,” akasema Bw Buli.
Naye Bw Lova Kokoto, alisema wakati umewadia kwa serikali kutumia ndege ili kuwafikishia wakazi wa Basuba chakula.
Bw Kokoto alisema inashangaza kwamba maafisa wa usalama wanaoendeleza operesheni ya kutafuta magaidi wa Al-Shabaab kwenye msitu wa Boni wamekuwa wakiletewa chakula kwa ndege kila mara ilhali wakazi wakisahaulika.
“Serikali kila mara huwaletea chakula wanajeshi na polisi wetu wanaodhibiti usalama eneo hili kupitia ndege. Sisi pia tunahitaji msaada wa dharura wa chakula hapa. Watumie hizo ndege kutuletea chakula. Tunaumia,” akasema Bw Kokoto.
Kwa upande wake, Bw Abubu Alali aliilaumu serikali kwa kukatiza ghafla mpango wa kuwasambazia Waboni chakula cha msaada na mahitaji mengine ambayo wakazi walikuwa wameahidiwa awali wakati serikali ilipozindua Operesheni ya Linda Boni mnamo 2015.
“Tuliahidiwa kwamba tungesaidiwa kwa chakula na misaada mingine hadi pale operesheni ya Linda Boni itakapositishwa. Hatuelewi kwa nini serikali imekatiza mpango huo,” akasema Bw Alali.
Tangu jadi, jamii ya Waboni imekuwa ikitegemea maisha ya msituni, ambapo wao huchuma matunda, kuwinda wanyama pori na kuvuna asali ya msituni.
Aidha tangu serikali ilipozindua operesheni ya Linda Boni kwa madhumuni ya kuwafurusha Al-Shabaab ndani ya msitu huo, jamii ya Waboni haijaruhusiwa kuendeleza shughuli zozote kwenye msitu huo.