Kimataifa

Nitapigania Waganda hadi kaburini, aapa Bobi Wine

September 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

Mwanasiasa wa Uganda Bobi Wine ameshikilia kuwa ataendelea na vita vya kukomboa nchi ya Uganda hata ikiwa inamaanisha afe.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kwa umma kwa mdomo alipofanyiwa mahojiano na kituo cha BBC Alhamisi tangu alipokamatwa na kusukumiwa mateso na serikali ya Rais Yoweri Museveni, Bw Wine aliwataka wananchi wa Uganda kujitolea katika vita hivyo akiwarai wasife moyo.

Kwenye ujumbe wake kwa vijana, mbunge huyo wa Kyadondo aliwataka kupigania kile wanachoamini kuwa ni haki na kuendelea kupigania hadhi ya taifa lao.

“Nitaendelea kutoa wito kwa Waganda haswa vijana kusimama kutetea imani zao, wasife moyo kamwe na kuzidi kusukuma hadi wapate haki na hadhi wanayostahili,” akasema Bw Wine akiwa Marekani ambapo anaendelea kupokea matibabu.

Alisema kuwa vita hivyo itawabidi kupigana hata ikiwa ni kwa kuuawa, chini ya wiki mbili tu tangu alipotoka jela baada ya kukamatwa na askari wa nchi ya Uganda.

Ni jana tu ambapo mbunge huyo alisimulia mateso makali aliyopitia alipokuwa ndani, akisema alifinywa nyeti pamoja na mateso mengine makali kiasi cha kupoteza fahamu.

“Na ni vita ambavyo lazima tupigane aidha ikiwa tutashinda ama tutakufa tukijaribu,” akasema.

Mbunge huyo amekuwa mpinzani mkubwa wa Rais Museveni na matatizo yake na serikali yalianza Agosti 13 walipokuwa kwenye kampeni eneobunge moja huko Uganda kumpigia debe mgombea ubunge wa upinzani, wakati vurugu zilidaiwa kuibuka na gari la msafara wa Rais Museveni likatupiwa mawe.

Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo pamoja na Rais Museveni wamekana kuwa walimtesa Bw Wine, huku habari kutoka idara ya polisi kudai kuwa maafisa wake hawana ujuzi wa kufanya mateso aliyosema alisukumiwa Bw Wine.