• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Elachi alilia Jubilee imwokoe

Elachi alilia Jubilee imwokoe

Na BRIAN OCHARO

SPIKA wa bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi ametaja hatua ya wawakilishi wadi wa kaunti hiyo kumng’atua kutoka kiti chake kuwa kinyume cha sheria na kuomba chama cha Jubilee kuingilia kati kusuluhisha mizozo baina ya wanachama wake katika bunge hilo.

Bi Elachi alisema si vyema kwa maafisa katika bunge hilo kuishi kwa woga wa kuadhibiwa kila wanapokosa kufuata masharti ya watu Fulani ama kufanya maamuzi ya kuwafurahisha watu fulani. “Itakuwa si haki kuwa kila wakati tunapokuwa na suala la aina hiyo, wanachama wanaadhibiwa amakuondolewa kutoka kamati na kutishiwa kuwa hawatasafiri,” akasema Bi Elachi.

Alivitaka vyama vya kisiasa kuchunguza mambo yanayoadhiri bunge hilo na kujiuliza ikiwa ni vyema kwa wanachama wao kuishi na woga bungeni kuwa wataadhibiwa ikiwa hawafuati mkondo fulani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Ocean Beach ambapo kongamano la kujadili masuala ya maendeleo kwa kaunti kame (ASAL) mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi linafanyika, Bi Elachi alisema kuwa kila mwakilishi katika bunge la kaunti ana haki ya kumwandikia ikiwa anahisi kuwa hafanyi kazi yake ipasavyo.

“Niliteuliwa na chama cha kisiasa na hivyo nakiomba chama kuamua ikiwa kinahisi kuwa sifanyi kazi namna inavyostahili, niliyopewa na Jubilee basi niandikieni barua kwani naambiwa ni uamuzi wa chama,” akasema.

Bi Elachi alisema si vyema kwa mwanachama wa Jubilee kupitia matatizo ya aina hiyo, wakati chama kina mikondo muafaka ya kutatua mizozo. Alijitetea kuwa amekuwa akifanya kazi yake namna inavyostahili, na akihusisha viongozi haswa kiongozi wa wengi na wa wachache bungeni.

“Wakazi wa Nairobi wanateseka kutokana na matatizo mengi na umasikini na hivyo kama viongozi wa bunge tunafaa kuwa tukijiuliza namna tunaweza kusaidia kuinua maisha ya wakazi wetu. Hilo ndilo jambo la muhimu zaidi na ambalo linaathiri kaunti yetu,” Bi Elachi, ambaye aling’atuliwa na madiwani 103 Alhamisi akasema.

Aliwataka MCAs kuacha kufanya mzaha, wakati bado kuna kazi kubwa mbele yao ya kuwahudumia wananchi.

Alikosoa hatua ya madiwani kumg’atua kuwa ilikiuka sheria, kwani sababu waliyotoa ili kuruhusiwa kuandaa kikao maalum ilikuwa kujadili masuala ya kiuchumi yanayoathiri bunge hilo na serikali ya kaunti.

“Nilitia saini kuandaliwa kwa kikao spesheli ambacho kilifaa kutumika kujadili masuala ya kiuchumi yanayoathiri bunge la kaunti ya Nairobi na upande wa serikali ya kaunti. Kwa hivyo kuamua kujadili kuning’atua ilikuwa kinyume cha sheria,” akasema.

Alikana kuwa aliiandikia tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) kuwachunguza baadhi ya viongozi wa bunge hilo kwa tuhuma za ufisadi, ambacho kinakisiwa kilisababisha kuondolewa kwake.

“Nilichofanya ni kuiomba EACC kuipa nguvu kamati ya bunge kuhusu kazi, nguvu na uwezo wa kuchunguza madai ya ufisadi bungeni na kuipa ripoti na adhabu itakayotoa,” akasema.

Aidha, alikana kutumia nafasi yake kupokea zabuni za bunge la kaunti.

You can share this post!

MAUAJI YA SHARON: Gavana Obado atoweka machoni pa umma

Nitawapa ‘Miguna’ mwingine, Sonko aonya...

adminleo