Habari MsetoSiasa

Nitawapa 'Miguna' mwingine, Sonko aonya wanaompa shinikizo

September 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

GAVANA wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ametahadharisha wanaomsukuma kuteua naibu wake, akiwataka kutompa ‘presha’ la sivyo ateue ‘Miguna mwingine’.

Gavana Sonko, ambaye miezi michache iliyopita alimteua wakili mtatanishi Miguna Miguna kuwa naibu wake wakati Bw Miguna akiwa Canada baada ya kutimuliwa humu nchini, sasa amesema akizidi kusukumwa, atafanya uteuzi mwingine wa aina hiyo ili apate muda zaidi wa kufikiria.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka mitatu tangu kufariki kwa babake, gavana huyo alisema kwamba anafaa kupewa muda kushauriana na chama cha Jubilee kabla ya kufanya uamuzi mwingine usio na msingi.

“Mimi nilichagua naibu wa gavana miezi michache iliyopita, jina likaenda katika bunge la kaunti na kutupiliwa mbali, sasa ningependa mnipe muda wa kutafuta ushauri kwani sitaki kuleta mtu hapa anisumbue,” akasema Gavana Sonko mnamo siku ya Alhamisi.

Gavana huyo alisema kwamba anahitaji muda kushauriana na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na maafisa wa Jubilee kabla ya kufanya uamuzi.

Alikosoa wanaomharakisha kuteua naibu wake kuwa hataki kusumbuliwa kwa sasa, ama wakizidi awape dawa yao ndipo apate muda zaidi.

“Kwa sababu mimi ni mtu wa Jubilee nashauriana na chama na Rais. Saa hivi hakuna ‘presha’, ule wakati walinipa ‘presha’ niliwapatia Miguna. Mimi sitaki kupewa presha kwa sababu nikipewa presha nitawaletea Miguna mwingine mmuangushe kwa hivyo tutangoja Rais arudi tushauriane,” akasema Sonko.

Mwezi mmoja uliopita, Gavana Sonko alichapisha majina manne ya wanawake kwenye ukurasa wake wa Facebook akisema ndio alioafikia kuwa bora na kuongeza kuwa alikuwa amewasilisha majina yao kwa chama cha Jubilee.

Hata hivyo, bunge la kaunti lilipuuzilia mbali hatua yake likisema alikuwa akifanya hila ili kupata muda zaidi, badala ya kuwasilisha jina la mteuliwa kukaguliwa.

Hata hivyo, katika hafla hiyo ya Alhamisi, Sonko aliandamana na msaidizi wa Kenyatta Jomo Gecaga ambaye alidokeza kuwa huenda akamteua.

“Hata yeye ningependa awe naibu wa gavana lakini bado tunashauriana,” akasema Gavana Sonko alipokuwa akimjulisha kwa wageni.