Kimataifa

Rais wa Sudan awapiga kalamu mawaziri wote

September 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA NA PETER MBURU

KHARTOUM, SUDAN

Rais wa Sudan Omar al-Bashir amefuta mawaziri 31 wa nchi hiyo na kuteua Waziri Mkuu mpya ambaye ataunda serikali mpya itakayosuluhisha matatizo ya kiuchumi taifa hilo.

Hatua hiyo ya Rais Bashar ilidhibitishwa na maafisa wakuu wa chama cha NCP baada ya vikao vya hadi usiku mkuu.

Hii ni kufuatia matatizo tele ya kiuchumi nchini Sudan, kutokana na upungufu mkubwa wa pesa za kigeni na kupanda kwa mfumko wa bei hadi asilimia 65.

“Hali ya uchumi inafaa kusuluhishwa na kwa sababu hii Rais Bashir akaamua kupunguza serikali katika sekta zote. Ameamua kuwa na serikali ndogo ya wanachama 21,” akasema Faisal Hassan Ibrahim, msaidizi wa ngazi ya juu wa Rais huyo baada ya mkutano.

Waziri Mkuu mpya sasa atakuwa aliyekuwa waziri wa unyunyiziaji maji katika baraza la mawaziri lililoondoka Moutaz Mousa Abdallah, huku aliyekuwa katika wadhifa huo Bakri Hassan Saleh akiteuliwa kuwa naibu wa Rais wa kwanza.

Rais Bashir aidha alimteua Mohamed Osman Yousif Kiber kuwa naibu wake.

Ibrahim said Abdallah alipewa jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri.

Mapema Jumapili, afisi ya Rais ilitangaza hatua ya Rais kufuta kazi serikali iliyoongozwa na Saleh katika kile ilichotaja kuwa “kurekebisha hali inayokumba taifa.”

“Ataunda serikali ambayo kwa mara nyingine itarejesha Imani ya watu wa Sudan” afisi ya Rais ikasema.

Hali ya uchumi ya Sudan imezorota, huku bei ya vyakula ikipanda maradufu, huku pesa za nchi hiyo zikipoteza ubora zikilinganishwa na dola ya marekani.

Benki kuu ya taifa hilo imepunguza ubora wa pesa za huko mara mbili mwaka huu, ukifikia pauni 28 kwa dola ya marekani

Hatua hii ya sasa inakuja miezi michache baada ya Rais Bashir kumtimua waziri wake wa masuala ya nje Ibrahim Grandour alipotangaza wazi kuwa wizara yake ilikuwa imeshindwa kulipa wafanyakazi, na mabadiliko ya wizara yaliyofuata baadaye.

Licha ya Marekani kuondoa vizingiti vya kibiashara nan chi hiyo Oktoba mwaka uliopita, hali ya kiuchumi ya Sudan bado imekuwa ikiyumbayumba.

Tangu Sudan Kusini kupata uhuru 2011, Sudan ilipoteza zaidi ya robo tatu za rasilimali ya mafuta, huku mashirika makuu ya kimataifa yakirai taifa hilo kutafuta mbinu za kufufua uchumi wake.

Januari, Sudan ilishuhudia maandamano miongoni mwa raia wake baada kupandisha bei za vyakula, lakini serikali badala ya kusuluhisha iliwakamata baadhi ya wanaharakati walioongoza na wanasiasa wa upinzani.