• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Serikali ya Museveni ilikosea kumuua Kirumira – Bobi Wine

Serikali ya Museveni ilikosea kumuua Kirumira – Bobi Wine

NA PETER MBURU

Mwanasiasa wa Uganda Bobi Wine amelaumu serikali ya nchi hiyo kwa mauaji ya kinyama ya afisa mkuu wa polisi Muhammad Kirumira, ambaye alipigwa risasi usiku wa Jumamosi.

Bw Wine, ambaye jina lake haswa ni Robert Kyagulanyi kupitia mitandao yake ya kijamii Jumapili jioni alishikilia kuwa mauaji ya afisa huyo hayatasitisha vita vya ukombozi Uganda, akirudia tena kuwa watapigana hadi kifo.

“Ndugu yangu Afande Kirumira, leo hii unalazwa ukiwa na miaka 35 pekee huku bado najaribu kuwaza namna ulivyouawa kinyama. Kosa lako lilikuwa kuzungumza ukweli kwa uongozi tu, kupigania haki na kupenda nchi yako,” akasema Bw Wine

Mbunge huyo wa Kyadondo ambaye yuko Marekani kwa matibabu baada ya kuteswa alipokamatwa na polisi wan nchi hiyo alisema walikuwa na ndoto kuu kwa maendeleo ya taifa hilo linalozongwa na malalamishi ya uongozi mbaya.

Bw Wine alisema kuwa ni polisi waliomuua afisa huyo wa polisi ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Yoweri Museveni.

“Ulikuwa umeketi pale Yasin awuma aliuawa na watu haohao tu ambao tunawalipa kutulinda,” akasema.

“Wamekuua lakini hawajasimamisha vita, ni vyema kufa ukipigana kuliko kuishi kama mtumwa, hatutawahi kufa moyo na hatutakuaibisha. Ni aidha tuwe huru ama tufe tukijaribu.”

Polisi wa Uganda Jumapili walitangaza mauaji ya afisa huyo ambayo yalitendeka eneo la Bulenga, wilaya ya Wakiso.

Kabla ya mauaji yake, Bw Kirumira alikuwa ameelezea hofu kuhusu vitisho dhidi ya maisha yake.

You can share this post!

Rais wa Sudan awapiga kalamu mawaziri wote

Senegal vs Madagascar: Shabiki afariki kabla ya mechi

adminleo