Uhuru apendekeza ushuru wa mafuta upunguzwe hadi 8%
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA watapata afueni kidogo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupendekeza kupunguza ushuru kwa mafuta kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8, hatua ambayo itapunguza bei ya bidhaa za mafuta, ikiwa itaidhinishwa na wabunge.
Kwa mfano, bei ya mafuta ya petroli itapungua kutoka Sh127 sasa hadi Sh118 kwa lita moja huku dizeli ikipungua kutoka Sh116 hadi Sh107.
Akihutubia taifa Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi Rais Kenyatta alisema alitoa pendekezo hilo baada ya kusikia kilio cha Wakenya waliolalamikia kupanda kwa gharama ya maisha tangu Septemba 1 serikali ilipoanza kutoza ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya asilimia 16 kwa bidhaa mafuta.
“Nimekuwa nikisikiza maoni kutoka Wakenya wa matabaka mbalimbali. Na ni wazi kuwa mmekerwa na madhara yanayotokana na ongezeko la bei za bidhaa za mafuta, na athari zake kwa gharama ya maisha. Ndio maana nimependekeza kwenye taarifa yangu kwa bunge, kupunguzwa kwa VAT ya mafuta kwa asilimia 50- kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8,” Rais Kenyatta akasema.
Aliwataka wafanyabiashara kutaendelea kuwanyanyasa Wakenya kutokana na bei za juu za bidhaa na huduma endapo bunge litaidhinisha pendekezo lake wiki ujao.
Rais Kenyatta alisema alikataa kutia saini Mswada wa Fedha, ambao wabunge waliufanyia mabadiliko kwa kupendekeza kuwa VAT kwa mafuta ianze kutekelezwa mnamo 2020, kwa sababu ya gharama kubwa ya kuendesha serikali.
“Gharama hiyo imechangiwa kupanuka kwa muundo wa serikali na ongezeko la nafasi za uwakilishi kama ilivyopendekezwa na Katiba ya sasa. Hii ni kando na hitaji la serikali la kufadhili miradi ya maendeleo na mipango ya kufaidi katika sekta za elimu na afya,” akasema.
Kando na kupunguza ushuru wa VAT kwa mafuta, Rais Kenyatta pia alisema Serikali itapunguza matumizi yake katika Wizara zote ili kufidia fedha ambazo itapoteza kufuatia hatua hiyo.
“Kwa sababu hatua hiyo haitoshi, pia nimependekeza kwenye taarifa yangu kwa bunge kwamba bajeti ya malazi, safari za humu nchini na nje, semina, warsa na mambo mengine yasiyo ya lazima katika wizara na idara za serikali ipunguzwe,” Rais Kenyatta akasema.
Hata hivyo, hakutaja Wizara au Idara za Serikali ambazo zitaathiriwa na hatua hiyo, endapo itaiodhinishwa na bunge wiki ujao litafanya vikao viwili kushughulikia mapendekezo yake.
Kulingana na Wizara ya Fedha, Serikali inalenga kukusanya Sh35 bilioni kutokana ushuru wa VAT kwa mafuta katika mwaka huu wa kifedha (2018/2019), kiasi ambacho sasa kitapungua hadi Sh17.5 bilioni.
Pengo hilo litajazwa na fedha ambazo zitakatwa kutoka katika Wizara zingine katika kile Rais alisema ni hatua ya “kusawazisha bajeti”.
Hata hivyo, Rais alipendekeza kwamba bajeti Idara ya mahakama na taasisi za kupambana na ufisadi iongezwe “ili kuimarisha vita dhidi ya ufisadi.”
“Vile vile, nimependekeza ongezeko la fedha kwa Idara ya Mahakama na taasisi za kupambana na ufisadi kama afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na ile ya kupambana na ufisadi (EACC), “ akasema.
Wakati huo huo, Rais Kenyatta jana alitetea hatua ya serikali yake kuongeza ushuru akisema hali hiyo imechagiwa na Katiba ya sasa ambayo imebuni nyadhifa zaidi za utawala na uwakilishi.
Alisema Katiba hiyo ambayo ilizinduliwa Agosti 27, 2010 imebuni mabunge mawili katika ngazi ya kitaifa na mabunge 47 katika ngazi ya kaunti kando pamoja na tume 16 za kikatiba, kando na idara ya mahakama, zinazoendeshwa kwa gharama kubwa.
“Chini ya katiba ya sasa mawanda ya demokrasia imepanuliwa sawa na muundo na utendakazi wa serikali. Sasa tuna mabunge mawili na idadi ya wabunge katika bunge la kitaifa imepanda kutoka 290 hadi 349 huku bunge la seneti likiwa na wanachama 67.”
“ Vile vile, tuna magavana 47, manaibu gavana 47 na mabunge ya kaunti yenye zaidi ya wanachama 1,000, wote hawa wanafadhili kwa pesa za ushuru wenu,” akasema alipohutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi.
Hata hivyo, Rais Kenyatta alisema serikali yake inajivunia hali kwamba imeweza kutekeleza Katiba kwa wakati na kufanikisha utekelezaji wa ugatuzi kwa manufaa wa Wakenya.
“Tumetuma zaidi ya Sh1 trilioni kwa serikali za kaunti tangu mwaka wa 2013, pesa ambazo zimetumika kuimarisha utoaji huduma, utekelezaji wa maendeleo na uimairishaji wa maisha ya Wakenya,” akasema.
Rais Kenyatta alisema hiyo ndio maana serikali yake itaendelea kulinda na kutetea ugatuzi chini ya muktadha wa katiba ya sasa bila kujali gharama.
“Kando na kufanikisha ugatuzi, kugharamia nyadhifa za uwakilishi, ushuru mnaolipa pia hutumika kuendeleza jenda faafu za maendeleo,” akasema.
Wanasiasa, viongozi wa kidini na Wakenya wa matabaka mbalimbali wamekuwa wakitoa wito Katiba hii ifanyiwe mabadiliko ili kupunguza nyadhifa za uwakilishi na utawala, kama njia ya kupunguza mzigo wa mishahara katika sekta ya umma.