Habari MsetoMakala

Umasikini unawasukuma mabinti kushiriki ngono wapate sodo – UNICEF

September 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PAUL REDFERN

IDADI kubwa ya wasichana wanaoishi katika mitaa ya mabanda kama vile Kibera jijini Nairobi wanalazimika kushiriki ngono ili wapate sodo.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (UNICEF) inaonyesha kuwa asilimia 65 ya wasichana wanabadilishana ngono na sodo kutokana na umaskini.

Katika utafiti huo wa UNICEF, asilimia 65 ya wasichana mtaani Kibera walikiri kuwa walikubali kushiriki ngono ili wapate pesa za kununua sodo.

Wasichana kadhaa katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya pia walisema kuwa wamewahi kushiriki ngono ili kupewa sodo na wanaume.

Wengine walisema wanalazimika kutumia nguo kuukuu, blanketi, magazeti, matope na manyoya ya kuku wakati wa hedhi.

Afisa Mkuu wa Maji na Usafi katika shirika la Unicef, Andrew Trevett, aliambia gazeti la Independent nchini Uingereza kuwa wengi wa wasichana hao wanafanya mapenzi na wahudumu wa bodaboda ambao huwapa sodo.

“Haya yanafanyika kutokana na umaskini na wengi wao hawana uwezo wa kununua sodo. Kadhalika, kuna uhaba wa sodo katika maeneo ya vijijini hivyo kulazimisha wasichana kutumia mbinu mbadala,” akasema.

Trevett pia alisema utamaduni wa jamii mbalimbali nchini Kenya unazuia watu kuzungumzia suala la hedhi hadharani, nyumbani au shuleni hivyo kusababisha wasichana kutumia njia za mkato kupata sodo.

Ripoti iliyofadhiliwa na Wakfu wa Bill & Melinda Gates Foundation mnamo 2016, ilibaini kuwa ni asilimia 50 pekee ya wasichana wanaoweza kuzungumzia wazi suala la hedhi nyumbani au shuleni.

Wasichana zaidi ya asilimia 75 waliohojiwa katika utafiti huo walisema pia wanahangaika kupata maji na sabuni wakati wa hedhi.

Ni asilimia 17 pekee ya wasichana waliosema kuwa kuna maji na sabuni shuleni kwao.

Ripoti ya Unicef inasema kuwa asilimia 30 ya shule zilizochunguzwa zinatoa sodo kwa wasichana wakati wa hedhi.

Alisema imani potovu zinazohusishwa na hedhi pia zinasukuma wasichana kutumia njia zisizofaa kujipatia sodo na hata sabuni.

“Kuna imani potovu kwamba hedhi hufanya mtu kuwa mchafu au ni mkosi au laana. Katika baadhi ya jamii msichana haruhusiwi kwenda jikoni wakati wa hedhi. Wengine pia wanaamini kwamba mazao yatanyauka shambani iwapo msichana mwenye hedhi atakanyaga shambani,” akasema.

Lakini kicha ya changamoto hizo zote, Shirika la Unicef linasisitiza kuwa Kenya imepiga hatua katika utoaji wa sodo kwa wasichana shuleni.

Ripoti inasema jumla ya wasichana 90,000 katika shule 335 wanapata sodo na vifaa vingine vya usafi kama vile sabuni.

Mwezi uliopita Rais Uhuru Kenyatta alitia saini sheria ambayo sasa itawezesha wasichana shuleni kupewa sodo bila malipo.