TAHARIRI: Madiwani wakome kutatiza maafisa
NA MHARIRI
KUMEKUWA na ripoti mbalimbali kuhusiana na viongozi wa kaunti, wakiwemo magavana, maspika na mawaziri, viongozi wa wengi au wachache katika mabunge ya kaunti kutishwa na madiwani wanapokataa kutimiza matakwa yao ya kibinafsi.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi na Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Embu Margaret Lorna Kariuki ndio waathiriwa wa hivi karibuni wa unyanyasaji huo wa madiwani.
Madiwani walidai kwamba Bi Elachi alifuja fedha za walipa ushuru kwa kuzuru ng’ambo kwa shughuli za kibinafsi na kutumia mamlaka yake vibaya na hata kukiuka maadili kwa mujibu wa katiba.
Jambo la kushangaza ni kuwa madiwani hao walimfurusha kwa nguvu Bi Elachi alipofika kazini hata baada ya korti kuagiza aendelee kuhudumu hadi kesi itakaposikilizwa.
Kinaya ni kwamba madiwani hao wamekimbia katika mahakama waliyopuuza agizo lake wakiitaka izuie Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kuwahoji kwa kufanya kitendo kinachokinzana na maadili ya uongozi.
Naye Bi Kariuki alitimuliwa kutoka wadhifa wake kutokana na madai kwamba alizembea na hata kusababisha mgawanyiko miongoni mwa madiwani.
Katika Kaunti ya Nyandarua, madiwani pia walijaribu bila mafanikio kutimua mawaziri wawili wa serikali ya Gavana Francis Kimemia kutokana na madai kwamba walikuwa na kiburi.
Madiwani wa Taita Taveta pia wanapanga kumtimua spika wao, karani wa bunge la kaunti na kiongozi wa wachache. Kisumu pia wamekuwa wakijaribu kumtimua Spika wao Onyango Oloo.
Ni kweli kwamba madiwani wana mamlaka ya kikatiba kumtimua spika wao. Madiwani vilevile, wana jukumu la kuhakikisha kuwa fedha za kaunti zinatumiwa kwa njia ifaayo. Lakini mamlaka hayo hayafai kutumiwa kiholela kwa tamaa za kibinafsi.
Madiwani wanastahili kuelekeza nguvu zao katika utungaji wa sera na sheria zitakazowezesha kaunti zao kustawi kiuchumi na wala si kutumia nafasi zao kujitafutia ubabe wa kisiasa.
Huu ni mwaka wa sita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi nchini na wananchi wangali wanangojea kwa hamu na ghamu matunda ya serikali za kaunti. Miaka mitano ya kwanza ilichukuliwa kuwa ya kujaribu mfumo wa ugatuzi na sasa ni muhula wa kuchapa kazi.
Wananchi wanahitaji maendeleo na wala si migogoro.