Kenya inaongoza Afrika Mashariki kwa vifo kutokana na kansa – WHO
Na JOHN MUTUA
KENYA ndiyo ina idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya saratani eneo la Afrika Mashariki, kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Kulingana na utafiti huo, saratani huua Wakenya 32,987 kila mwaka, hivyo asilimia 40 ya vifo 89,426 vinavyoripotiwa katika mataifa ya eneo la Afrika Mashariki Kenya Uganda na Tanzania.
Ripoti hiyo inayoitwa Globocan iliangazia visa vipya vya ugonjwa huo miongoni mwa wanaume na wanawake.
Tanzania iliorodheshwa ya pili kwa visa 28,610 huku Uganda ikiwa na visa vichache zaidi, vikiwa 21, 829 ama idadi ndogo tu zaidi ya asilimia 25 ya visa vyote vilivyoripotiwa katika mataifa yote matatu.
Saratani ya njia ya uzazi kwa wanawake (Cervix) ndiyo inayosababisha vifo vingi zaidi, ikichangia vifo 14,282, karibu mara mbili ya watu waliofariki kutokana na kiini cha pili cha vifo ambacho ni saratani ya koromeo (Oesophagus).
Saratani ya uume, matiti na Kaposi Sarcoma zilifungia idadi ya aina tano za ugonjwa huo zinazoongoza kwa kusababisha vifo katika mataifa hayo.
Humu nchini, saratani ya koromeo husababisha vifo vya watu 4,351 kila mwaka, idadi zaidi ya mara mbili ya idadi iliyoripotiwa Uganda.
Tanzania iliripoti visa 6,695 vya vifo, ama asilimia 46 ya jumla ya vifo vilivyoripotiwa eneo hili mwaka uliopita, kulingana na ripoti hiyo.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo imeorodheshwa na WHO kati ya majumuiya matano yaliyo na visa vya saratani ya njia ya uzazi ilianzisha kampeni ya kutoa chanjo katika kila taifa ili kudhibiti ugonjwa huo ambao hukumba wanawake.
Kampeni hiyo iliyoanza Aprili imekuwa ikiwapa wasichana kuanzia miaka 14 chanjo ya Human Papilloma Virus (HPC).
Uganda ndiyo inaongoza katika visa vya vifo vitokanavyo na saratani ya Kaposi Sarcoma, ambayo huvamia watu wenye udhaifu wa kujikinga dhidi ya magonjwa kama Ukimwi.
Nchi hiyo iliripoti vifo 2,159, karibu nusu ya 4,485 kwa jumla vilivyorekodiwa mwaka uliopita. Lakini saratani ya uteri bado inasalia kuwa aina ya ugonjwa huo ambayo inachangia vifo vingi nchini humo, vikiwa 4,301 kila mwaka.
Saratani ya kibofu (bladder) ndiyo inasababisha vifo vichache zaidi katika eneo zima kati ya aina 13 za ugonjwa huo zilizoorodheshwa, ikichangia vifo 1,230 kila mwaka.
Changamoto zinazokumba eneo hili katika kupambana na ugonjwa huo ni upungufu wa vifaa licha ya kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa na pesa chache za kujenga vituo zaidi vya matibabu ya ugonjwa huo.
Hospitali ya Kenyatta (KNH) ambayo ndiyo kubwa zaidi kimatibabu mashariki na kati mwa Afrika tayari imelemewa na visa vingi vya Wakenya wanaotafuta huduma za saratani katika kifaa hicho. Hospitali hiyo imelazimika kuhudumia wagonjwa wa kutoka mataifa jirani.
Ripoti hiyo, aidha, iliyonyesha wanawake wa Kenya ndio wako kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa saratani eneo hili, hali ya unene ikitajwa kama kichochezi kikuu.