• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wafuasi wa Obado sasa waandamana wakitaka aachiliwe huru

Wafuasi wa Obado sasa waandamana wakitaka aachiliwe huru

Na WAANDISHI WETU

WAFUASI wa Gavana wa Migori, Bw Okoth Obado Jumapili waliandamana katika barabara kuu ya Migori-Kisii kutaka aachiliwe huru, huku akitarajiwa kufikishwa mahakamani Nairobi leo kwa madai ya kuhusiana na mauaji ya Bi Sharon Otieno, aliyekuwa mpenzi wake na mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Rongo.

Waandamanaji hao walidai mashtaka dhidi ya Bw Obado yana msukumo wa kisiasa.

Walifanya maandamano hayo katika barabara za kituo cha kibiashara cha Uriri, kilicho katika barabara ya Migori-Kisii.

“Tunataka gavana wetu kuachiliwa kwa dhamana,” akasema Bw Michael Omollo, akiongeza kuwa hawawezi tena kuvumilia kuzuiliwa kwake.

Wakati huo huo, wafuasi wake wengi na wafanyakazi wa serikali ya kaunti ya Migori walisafiri hadi jijini Nairobi kumtia moyo atakapofikishwa mahakamani.

Wafuasi hao waliondoka Migori mnamo Jumamosi usiku kwa magari ya uchukuzi wa umma, ya kibinafsi na wengine wakasafiri kwa ndege.

Walisema kwanza wangemtembelea Bw Obado katika Kituo cha Polisi cha Gigiri alikozuiliwa ambapo baadaye wataungana naye mahakamani.

Hata hivyo, polisi wameshikilia kwamba watakaoruhusiwa kumwona ni jamaa na mawakili wake pekee. Vile vile, wanaeleza kuwa hataruhusiwa kupelekewa chakula kutoka nje ya seli.

Wafanyakazi hao wanaojumuisha mawaziri, wakuu na wakurugenzi wa idara mbalimbali walisema kwamba wanaomba Mungu gavana huyo apewe dhamana ili kumruhusu kurejelea majukumu yake.

“Tunatarajia kwamba kiongozi wetu atahimili mawimbi haya ili kumwezesha kurejelea ajenda zake za maendeleo. Tungetaka kuuhakikishia umma kwamba shughuli za kaunti zinaendelea kama kawaida licha ya kukamatwa kwake,” akasema Bw Elijah Odhiambo, ambaye ndiye Waziri wa Ardhi.

Baadhi ya wanachama wa Ukoo wa Kanyamkago, anakotoka Bw Obado pia walisafiri Nairobi kumwunga mkono.

“Tunatarajia kwamba taratibu za kesi yake zitaharakishwa bila uingiliaji wowote wa kisiasa. Tunafuatilia suala hili kwa karibu ili kuhakikisha kuwa kanuni zote za kisheria zimezingatiwa,” akasema George Owino, ambaye ndiye mwenyekiti wa ukoo wa Kanyamkago.

Alisema kuwa Bw Obado anakabiliwa na hali ngumu sana, hivyo na anahitaji maombi kutoka kwa Wakenya wote wa heri njema.

Kando na hayo, Bw Owino aliwaomba watumizi wa mitandao ya kijamii kuacha kumhukumu Bw Obado kabla taratibu za kisheria kukamilika.

Bw Obado alikamatwa mnamo Ijumaa kuhusiana na mauaji wa Sharon.

Washukiwa wanne, wakiwemo wasaidizi wake wa kibinafsi na mlinzi pia wanazuiliwa na polisi. Hao ni Michael Oyamo (msaidizi), Jack Gombe (dereva wa teksi), Elvis Okoth (mlinzi), Lawrence Mula (mwanasiasa) na Obiero (msaidizi)

You can share this post!

MSALITI AU MZALENDO: Jinsi kuwa Raila Odinga si kazi rahisi

Uhuru akwepa ghadhabu za Wakenya walio Amerika

adminleo