Makala

ZIWA NAIVASHA: Kivutio cha utalii kilichogeuka mtego wa mauti

September 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MAOSI NA MACHARIA MWANGI

VIBOKO katika Ziwa Naivasha wanaoaminika kuwavutia watalii wengi, sasa si fahari ya wakazi tena kwani wamegeuka kuwa tisho  kwa utalii na maisha ya binadamu.

Mauti ya hivi punde yalimfika mtalii kutoka Taiwan aliyekuwa akijivinjari katika fuo za ziwa hilo. Hii imeongeza idadi ya waathiriwa wa mashambulizi ya viboko.

Mtalii mwenyewe alikuwa akifanya utafiti katika ziwa hilo mchana kutwa lakini jua lilipotua, ndipo maisha yake yalipokatizwa asijue hangerejea kwao akiwa mzima tena.

Mwenzake alinusurika kifo baada ya kupata majeraha mabaya,lakini hatimaye  maafisa wa kitengo cha wanyama pori walifanikiwa kuangamiza kiboko huyo.

Jambo hili liliwakasirisha wavuvi na wahudumu katika ziwa wakililia idara husika kuwahakikishia usalama wao katika harakati zao za kila siku wakisaka riziki.

Mkasa huu uliotokea mwezi uliopita, unaashiria ukosefu wa usalama ziwani humo kwani mnamo 2013 mzee mmoja aliyekwenda ziwani kuteka maji pia aliangamizwa akiwa ufuoni.

Taswira kamili katika eneo la tukio inaelezwa na Enoch Romano 26 aliyepoteza miguu yote katika mtaa wa Kasarani, kaskazini ya Ziwa Naivasha.

Enoch Romano aliyeshambuliwa na kiboko akiwa katika ufuo wa Ziwa Naivasha na kupoteza miguu yote miwili. Picha/ Macharia Mwangi

Tukio hili la 2018 lilitokea mwendo wa saa nne asubuhi ambapo yeye na rafiki zake walishuka kutoka kwenye mashua yao kutafuta kuni kandokando ya ziwa bila kujua  wanaviziwa kutoka mbali na wanyama hatari.

”’Ghafla kiboko alitokea vichakani na kabla sijakimbia alining’ata na kuniacha hoi taabani,” anaeleza tukio hilo la kushtua.

Tulipomzuru anapoishi katika mtaa wa Kasarani, tulikaribishwa na hali tete ya huzuni pamoja na utulivu usiokuwa wa kawaida.

Enoch akijaribu kurudia hali yake ya zamani, ulemavu umeshamwandama, na kupigilia msumari moto katika kidonda mkewe alimtoroka, mama mtoto wa miaka sita.

Kinachouma zaidi aliolewa na jirani yake tena rafiki wa siku nyingi kwa familia, takriban mita 600 kutoka anapokaa.

“Nilijaribu kila mbinu kumrudisha nyumbani bila mafanikio, na badala yake nikapokea kichapo cha mbwa kutoka kwao,” Romano alisema huku akijaribu kuficha machozi yake.

Manusura mwingine alifikishwa hospitalini kutokana na majeraha ya kiboko kutoka mtaa wa Kamere lakini siku chache baadaye akaishia kufa akipokea matibabu.

Eneo hilo la Kasarani lenye matukio mengi pia liliandikisha tukio jingine ambapo mwathiriwa kwa jina Manyara alishambuliwa. Taifa Leo Dijitali ilipotafuta makazi yake rasmi kumhoji, ilikuta tayari asharudi kwao mashambani.

Japo hakuwa amepona vizuri majirani walieleza alipata majeraha mabaya ya mgongo.

Kulingana na msimamizi wa shughuli za mashua katika Ziwa Naivasha Bw David Kilo, kuna mtu mwingine aliyezikwa wiki iliyopita kutokana na mashambulizi.

Mvuvi mashuhuri David Kilo akiwa katika ufuo wa Ziwa Naivasha. Picha/ Macharia Mwangi

“Kwa miaka 30 nimekuwa nikihudumu katika ziwa hili. Nimeshuhudia zaidi ya watu 100 wakiangamizwa na viumbe hawa hatari wasiokuwa na huruma,” Bw Kilo alisema.

Hata hivyo analaumu walowezi wa kibinafsi na mabwenyenye walionyakuwa sehemu ya ardhi ya ziwa na kuifanya makazi ya watu.

“Viboko hawapati uhuru wa kutosha wanapotoka majini wakielekea kwenye ardhi kusaka chakula. Wao huishia kukutana na binadamu wasiokuwa na habari na kutekeleza maangamizi,” Bw Kilo alisimulia.

Alieleza kwamba viboko ndio kivutio kikubwa cha watalii katika Ziwa Naivasha. Bila hao hakuna shughuli ya utalii itakayoendesha katika eneo hilo.

“Tusijidanganye kwani bila viboko basi utalii wa ziwa hili utakuwa umefifia na kukosa mashiko yake,” alisema.

Anapendekeza maafisa zaidi wenye ujuzi wa kutosha waajiriwe na idara ya kulinda wanyama pori ili kuongeza usalama kwa wakazi na watalii.

Aliwarai wavuvi pia kuzingatia kanuni ya kutovua usiku wasije wakayahatarisha maisha yao kutokana na idadi kubwa ya viboko wanaozurura usiku wakisaka lishe.

Jeremiah Oloo pia ni mvuvi wa tajriba pana na amekuwa akihudumu kwa miaka mingi katika ziwa Naivasha na anafahamu mengi kuhusu mikasa hii.

Alieleza kwamba japo baadhi ya visa vimeripotiwa bado kuna watu wengi katika makao yao wanaendelea kuuguza majeraha kimyakimya bila kutoa taarifa kwa umma.