Sikumuua Sharon, Obado aambia mahakama
Na RICHARD MUNGUTI
BAADA ya siku nyingi za sintofahamu, hatimaye Gavana wa Migori Bw Zachariah Okoth Obado (pichani) alishtakiwa kwa mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Bi Sharon Beylen Otieno hapo Jumatatu.
Bw Obado alifikishwa mbele ya Jaji Jessie Lessit, katika mahakama kuu ya Milimani Nairobi. Akiwa amevalia suti ya rangi ya buluu alifikishwa mahakamani mwendo wa saa tatu asubuhi na kurudishwa rumande hadi saa tano asubuhi.
Jaji Jessie Lessit alimsomea Bw Obado mashtaka baada ya kukabidhiwa cheti cha kuthibitisha Bw Obado alikuwa mwenye akili timamu na anaweza kujibu mashtaka.
“Mshtakiwa amepimwa akili?” Jaji Lessit alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bw Jacob Ondari.
“Ndio, mshtakiwa alipimwa na mtaalamu wa tiba ya ubongo na kuthibitishwa kuwa mwenye akili timamu,” alijibu Bw Ondari huku akimkabidhi Jaji Lessit.
Baada ya Bw Obado kukanusha shtaka dhidi yake, Jaji Lessit aliamuru mshtakiwa azuiliwe katika gereza la eneo la Viwandani, Nairobi hadi uamuzi utakapotolewa ikiwa ataachiliwa kwa dhamana au la.
Jaji Jessie Lessit aliamuru Bw Obado azuiliwe katika gereza hilo baada ya kukataa ombi la mawakili wake Cliff Ombeta, Jaji Nicholas Ombija na Rodgers Sagana azuiliwe katika kituo cha Polisi cha Gigiri.
Jaji Lessit alitupilia mbali ombi la mawakili hao watatu wanaomtetea Gavana huyo wa Migori aliyekanusha shtaka la kumuua Bi Sharon Otieno katika eneo la Owade kaunti ndogo ya Rachuonyo usiku wa Septemba 3, 2018.
Mawakili hao waliomba mahakama iamuru azuiliwe katika kituo cha polisi cha Gigiri ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana likisubiri kuamuliwa.
“Naomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana. Tumejadiliana na viongozi wa mashtaka Mabw Jacob Ondari na Tom Imbali kuhusu kuachiliwa huru kwa dhamana kwa mshtakiwa . Tumewapa viongozi hawa wa mashtaka nakala ya ombi letu la dhamana. Ikiwa hawapingi mwachilie mshtakiwa kwa dhamana,” alisema Cliff Ombeta.
Bw Ombeta alimweleza Jaji Lessit kuwa mawakili wanaomtetea mshtakiwa walikuwa tayari kuwasilisha ombi hilo.
Bw Ondari aliambia mahakama kuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Bw Noordin Haji amepinga Gavana Obado akiachiliwa kwa dhamana.
“Polisi hawamhitaji tena Bw Obado kwa vile ameshtakiwa kwa mauaji ya Bi Otieno. Amekanusha shtaka. Sasa anatakiwa kuwekwa chini ya uangalizi wa maafisa wa idara ya magereza,” Bw Ondari alifafanua.
Aliambia mahakama kuwa mshukiwa wa mauaji awaye yeyote akisha kana mashtaka , makazi yake huwa ni gerezani chini ya uangalizi wa askari jela.
Bw Ondari alisema anahitaji muda awasiliane na afisa anayechunguza kesi hiyo awasilishe afidaviti ikisimulia sababu za kukataa Bw Obado akichiiliwa kwa dhamana.
Bw Ombija alimweleza Jaji Lessit kuwa Bw Obado alitiwa nguvuni Ijumaa na amekuwa ndani tangu siku hiyo.
Jaji Lessit aliamuru ombi la dhamana la Bw Obado lisikizwe leo saa nane.
Awali mahakama ilikuwa imeombwa isikize ombi hilo la dhamana kesho (Jumatano) wakati kesi dhidi ya msaidizi wake Obado, Bw Michael Oyamo itakapotajwa.
Miongoni mwa waliofika kusikiza kesi hiyo ni mama yake Sharon. Baada ya kuagizwa azuiliwe gereza la Viwandani, wafuasi walipinga kushtakiwa kwa Bw Obado wakimlaumu mwendazake kwa kuchangia kufariki kwake.