Habari MsetoSiasa

Siogopi kuvuliwa mamlaka, Mbadi aambia wabunge wanaomtishia

September 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi amewataka wabunge wa upinzani wanaomkashifu kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono marekebisho yaliyopendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta katika mswada wa fedha 2018 uliopitishwa bungeni wiki jana kuendelea na mpango wao wa kumtimua kutoka wadhifa wake.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuchangisha fedha katika Kanisa Katoliki la Nyandiwa, Suba Kusini, Bw Mbadi alisema kwamba aliunga mkono kupunguzwa kwa ushuru wa VAT kwa bidhaa za petrol kutoka asilimia 16 hadi 8 ili kusaidia taifa kulipa madeni yanayodaiwa na mataifa ya kigeni.

‘Mimi ni mhasibu kitaaluma na nafahamu mambo kadhaa kuhusu bajeti. Siogopi vitisho vya kuning’oa katika wadhifa wa kiongozi wa wachache wala kuhukumiwa na mtu yeyote. Kenya lazima ingetafuta mbinu za kusawazisha hali ili kuyalipa madeni yake na wakati uo huo kugharamia matumizi ya kinyumbani,” akasema Bw Mbadi.

Aidha Mwenyekiti huyo wa chama cha ODM alifafanua kwamba serikali hukusanya Sh1.9 trilioni ambazo hazitoshi kulipa madeni hayo na vile vile kugharamia maendeleo ya nchi.

“Serikali ya kitaifa hutumia Sh640bilioni kulipa mishahara na Sh314 bilioni kufadhili ugatuzi kwenye kaunti zote 47. Kwa hivyo serikali huhitaji mbinu ya kusawazisha namna inavyosambaza fedha zake na kuyalipa madeni ikizingatiwa bado tuna upungufu wa Sh870bilioni kugharamia uendeshaji wa maswala ya nchi,” akaongeza Bw Mbadi.

Wakati wa mjadala huo mkali bungeni wiki jana, Bw Mbadi na kiongozi wa wengi Aden Duale walitajwa na wabunge wenzao kama wasaliti walipounga mkono mswada huo uliopingwa vikali na wengi wa wabunge kutoka mirengo yote ya Jubilee na Nasa.

Hata hivyo mbunge huyo wa Suba Kusini aliwakashifu baadhi ya wabunge wenzake kama ndumakuwili walipokosa kuyaibua maswala kuhusu mswada huo wakati wa mkutano wao na vinara wa vyama vya Jubilee na Nasa ambao ni Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Kutokana na kupashishwa kimabavu kwa mswada huo, wabunge walioupinga wametaka mabadiliko makubwa yatekelezwa kwenye uongozi wa bunge mojawapo ikiwa ni kuwatimua Spika Justin Muturi, Bw Mbadi na Bw Duale kutoka kwa nyadhifa zao.

Wakati wa hafla hiyo Bw Mbadi aliyekuwa ameandamana na madiwani15 wa kaunti za Homabay akiwemo kiongozi wa wengi Walter Muok aliwataka wawakilishi wa wadi kutekeleza jukumu lao la kuitia mizani serikali za kaunti ipasavyo ili kuzuia ubadhirifu wa fedha unaolemaza maendeleo mashinani.