• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Uganda yazuia Kenya kupandisha bendera kisiwani Migingo

Uganda yazuia Kenya kupandisha bendera kisiwani Migingo

NA MWANDISHI WETU

JUHUDI za maafisa wa Kenya kupandisha bendera katika Kisiwa cha Migingo ziliambulia patupu kwa mara nyingine mnamo Ijumaa iliyopita, baada ya maafisa wa Uganda kudai wenzao wa Kenya hawakufuata kanuni.

Mzozo kuhusu usimamizi wa kisiwa hicho ulizidi wiki iliyopita wakati ilipodaiwa maafisa wa Uganda walishusha bendera ya Kenya na kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi katika kisiwa hicho.

Hatua ya Uganda imesababisha taharuki miongoni mwa wavuvi wa Kenya, wengi ambao wameanza kuhama kisiwa hicho kwa kuhofia usalama wao.

Mwenyekiti wa Kundi Simamizi la Ufuo wa Migingo, Bw Gabriel Isaiah Ungwe, alisema aliona maafisa wa Kenya wakienda kupandisha bendera lakini wenzao wa Uganda wakawafuata na kusisitiza kanuni hazikufuatwa.

“Baadaye pande hizo mbili zilizungumza kujaribu kusuluhisha suala hilo. Maafisa wa Kenya kisha walisitisha juhudi zao na kufikia sasa hatujaona chochote. Afisa aliyekuwa amekuja kutoka Kaunti Ndogo ya Nyatike kupandisha bendera asharudi alikotoka,” akasema.

Bw Ungwe alisema maafisa wengi wa usalama kutoka Uganda wangai kisiwani humo.

“Kwa upande mwingine kuna maafisa 12 pekee wa polisi wa Kenya na wakati mwingine wanapoenda nyumbani kunaweza kusalia polisi wachache hadi watatu pekee.

Kamishna wa Kaunti ya Migori, Bw Joseph Rotich, alisema maafisa wa usalama wa Kenya kwa sasa wanaendelea kushauriana kuhusu amani kisiwani humo na wenzao wa Uganda, na kuna utulivu.

Alisema kuwa bendera ya Kenya itapandishwa Migingo hivi karibuni na akawataka Wakenya walio katika kisiwa hicho wasiwe na wasiwasi..

“Bendera haikupandishwa kwa sababu ya taharuki iliyosababishwa na idadi kubwa ya maafisa wa usalama wa Uganda walioletwa kisiwani. Lakini nawahakikishia shughuli hii itatekelezwa,” akasema Bw Rotich.

Aliongeza kuwa maafisa wa Kenya na Uganda wameelewana kuwa na mwongozo kuhusu jinsi maafisa wa usalama wanavyofaa kupelekwa kisiwani humo na kila nchi.

“Kwa sasa kuna utulivu. Wavuvi wa Kenya wanaendelea na shughuli zao za kawaida bila matatizo. Wale ambao walihama pia wamerejea,” akasema.

Mzozo kuhusu umiliki wa kisiwa hicho umekuwepo kwa miaka mingi kutokana na Kenya na Uganda kudai kukimiliki kisiwa hicho kidogo.

Mwezi jana Waziri wa Usalama, Fred Matiang’a alisema Kenya haitakubali raia wake kuendelea kuhangaishw na maafisa wa usalama wa Uganda.

Kisiwa hicho kimekuwa kikizozaniwa na nchi hizi mbili hasa kutokana na utajiri wake wa samaki na biashara zingine.

You can share this post!

Siogopi kuvuliwa mamlaka, Mbadi aambia wabunge wanaomtishia

Uhuru avumisha Kenya Airways nchini Amerika

adminleo