• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Mwanamke anayedaiwa kuwa na HIV taabani kwa kunyonyesha mtoto wa jirani

Mwanamke anayedaiwa kuwa na HIV taabani kwa kunyonyesha mtoto wa jirani

Na MERCY KOSKEY

MWANAMKE wa miaka 27 Jumanne alishtakiwa katika Mahakama ya Nakuru kwa madai ya kumwambukiza virusi vya Ukimwi mtoto wa miezi tisa wa jirani yake.

Mshtakiwa alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Joe Omindo ambapo alishtakiwa kwa kumnyonyesha mtoto huyo licha ya kufahamu kwamba ana virusi vya HIV.

Kulingana na mashtaka, mwanamke huyo alifanya hivyo bila kutilia maanani hatari ya kiafya aliyomweka mtoto huyo.

Mshtakiwa anadaiwa kufanya kitendo hicho Septemba 18 mwaka huu katika eneo la Gichobo, Kaunti Ndogo ya Njoro.

Kulingana na upande wa mashtaka, mamake mtoto huyo alimwachia ili amlindie mtoto huyo alipoenda kazini. Wawili hao ni majirani.

Hata hivyo, mlalamishi hakufahamu mshtakiwa ana virusi hivyo na hangemfanyia mtoto wake kitendo kama hicho.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa alianza kumnyonyesha mtoto huyo baada ya jaribio la kumtuliza kutofaulu.

Bi Njeri alipatikana na majirani waliojua hali yake akimnyonyesha mtoto huyo.

Alikamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Njoro.

Hata hivyo, alikanusha mashtaka hayo. Hakupewa dhamana yoyote huku mtoto huyo akiendelea kupokea matibabu.

Mahakama iliagiza awekwe rumande katika kituo hicho na kupokea matibabu kutokana na hali yake.

Kesi hiyo itatajwa tena hapo Oktoba 2.

You can share this post!

Wakenya sasa wamlilia Okiya Omtatah awakomboe, wamfadhili...

Idara yatabiri kutakuwa na mvua kubwa Pwani hadi Ijumaa

adminleo