• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Mkenya ashinda Sh100 milioni kwenye tuzo za Facebook

Mkenya ashinda Sh100 milioni kwenye tuzo za Facebook

Na BERNARDINE MUTANU

WAKENYA ni baadhi ya washindi wa tuzo za kijamii za Facebook. Mkenya Noah Nasiali alishinda Sh100 milioni katika shindano hilo baada ya kuchaguliwa kama mshindi Barani Afrika.

Hii ni baada ya kuwaleta pamoja wakulima 120,310 kutoka kote Afrika kujifunza kuhusu kilimo kupitia kwa ukurasa wake wa Africa Farmers Club kwenye Facebook.

Ukurasa huo uliundwa mwishoni mwa mwaka 2017 na ni miongoni mwa washindi watano wa kima hicho kutoka maeneo tofauti ulimwenguni.

“Kiwango cha mwisho cha tuzo hiyo kitaamuliwa kuambatana na bajeti ya mwisho katika ombi kama sehemu ya utoaji wa mafunzo,” ilisema Facebook kupitia kwa msimamizi wake Afrika Nunu Ntshingila.

Kulingana na kampuni hiyo, kilimo ni moja ya sekta muhimu zaidi Barani Afrika na habari kuhusu kilimo ni muhimu sana kwa ukuzaji wa sekta hiyo.

Katika tangazo, Facebook pia iliorodhesha Wakenya watano kama washindi wa Sh5 milioni kwa ubunifu wao katika mtandao wa Facebook.

Wakenya hao walikuwa kati ya watu 116 kote ulimwenguni ambao walichaguliwa kujiunga na kundi la Facebook la Uongozi wa Kijamii.

Watano hao ni Felister Wangari, mwanzilishi wa 52-Saving-Challenge, Pamela Oduor ambaye ni mwanzilishi wa Lets Cook Kenyan Meals, Asha Mweru-#WomenWorkKE, Caroline Kihusa, Still A Mum na Truphosah Monah, Women And Realities of Disability Society.

Wakenya hao walikuwa miongoni mwa Waafrika 11 walioshinda tuzo hilo lililotangazwa Jumanne.

“Viongozi wengi wa kijamii kote ulimwenguni na Afrika hutumia Facebook kuunda ushirika kupitia kwa makundi ya Facebook, Whatsapp na Messenger,” alisema Ntshingila.

Facebook ilikuwa ikizingatia athari za kila ukurasa katika jamii, na kusema waanzilishi wa kurasa hizo walihitaji rasilimali na usaidizi wa kifedha kwa lengo la kukuza azma zao na jamii.

Afrika Kusini ilikuwa na washindi watatu wa Sh5 milioni, Uganda (mmoja), Senegal (mmoja) na Nigeria(mmoja).

Programu hiyo itahudhuriwa na itashirikisha washiriki 100 na vijana ambao watapokea kufikia milioni tano kujikuza katika kuendeleza azma yao.

You can share this post!

HONGO BUNGENI: Wa Muchomba asimulia wabunge walivyomumunya...

Nitaunga mkono muafaka UhuRuto wakiomba radhi kwa kuiba...

adminleo