• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
TAHARIRI: Kampuni za kamari zifanyie spoti hisani

TAHARIRI: Kampuni za kamari zifanyie spoti hisani

NA MHARIRI

BAADA ya serikali kuzipunguzia kampuni za bahati nasibu ushuru kwa asilimia kubwa, itakuwa muhimu kampuni zote kubwa zitumie fursa hiyo kuanza kudhamini aina mbalimbali ya michezo humu nchini.

Matarajio yetu ni kwamba SportPesa ambayo imekuwa ikiongoza katika ufadhili wa michezo, hasa kandanda, itarejesha udhamini wake wote na labda zaidi, ambao ilikatisha au kupunguza serikali ilipoongeza ushuru kwa kampuni zote za bahati nasibu.

Kinachoumiza sekta ya spoti nchini Kenya kwa sasa ni ukosefu wa wadhamini. Katika dunia ya leo, bila udhamini maendeleo ya maana katika sekta hii hayawezi kupatikana. Hii ndiyo maana katika mataifa yaliyostawi, michezo huendeshwa kama biashara, hivyo basi kuziletea timu zinazoshiriki michezo hiyo pato la kutosha.

Inapozingatiwa kuwa michezo ni sekta kubwa inayoweza kuwa dawa mujarabu kwa uhaba wa kazi nchini, itakuwa aula fani hii ya maisha ipewe uzingativu zaidi. Uzingativu huu bila shaka ni kuzidisha udhamini maradufu.

Maadamu kwa sasa Kenya ina kampuni nyingi sana za michezo ya bahati nasibu ya spoti, inakuwa bora nyingi ya kampuni hizi zijitwike jukumu la kuinua hadhi ya soka nchini kwa kuzifadhili timu zetu, hasa zile za kijamii, kama vile AFC Leopards na Gor Mahia.

Mbali na soka SportPesa ilikuwa ikidhamini mchezo wa raga lakini ikaondoa punde ushuru ulipoongezwa hadi asilimia 35 kwa jumla ya mapato ya kampuni hizo. Lakini baada ya ushuru huo kurudishwa chini hadi asilimia 15 pekee, kampuni hizi hazina sababu ya kurejesha ufadhili huo kwa mchezo wa raga ambao umekuwa ukikumbwa na uchechefu wa kifedha.

Karibu tatizo la kifedha lisambaratishe kikosi cha taifa cha raga ya wachezaji saba kila upande msimu uliokamilika.

Mgogoro huo karibu umpokonye kocha tegemeo Innocent Simiyu wadhifa huo licha ya mkufunzi huyo kuandikisha rekodi ya alama nyingi zaidi ambazo Kenya imewahi kupata katika Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande.

Kwa sababu hiyo, kampuni hizi zina jukumu kwa jamii; kutumia sehemu ya faida zinayopata kuziba pengo la udhamini lililopo katika sekta ya michezo.

Tuna imani, kadhalika, kuwa mchango wa kampuni hizo unaweza kusaidia zaidi kuinua vipawa vya chipukizi nchini.

You can share this post!

Raia wa Argentina wagoma kulilia hali mbaya ya uchumi

Wawakilishi Wanawake hawana manufaa, wabunge wapunguzwe...

adminleo