RAILA ACHEMSHA RUTO
Na WAANDISHI WETU
UHASAMA wa kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga ulichipuka upya Jumapili.
Bw Ruto alimshambulia kiongozi huyo wa Chama cha ODM kwa maneno makali akiwa ziarani katika Kaunti ya Mombasa, ambako kumekuwa ngome ya Bw Odinga kwa miaka mingi.
Alidai Bw Odinga anatumia muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta kuvuruga Chama cha Jubilee ili kumng’oa yeye (Bw Ruto) katika chama hicho jinsi alivyofanyiwa akahama ODM baada ya uchaguzi wa 2007.
“Nilikuwa mwanachama wa ODM, wakajitahidi hadi wakahakikisha nimeondoka katika chama hicho na hata wakanipeleka mahakamani. Hayo ndiyo sasa wanataka kuleta katika Jubilee lakini nawaambia hawatatoboa,” akasema Naibu Rais.
Bw Ruto alionekana kukerwa na kauli ya Kiranja wa Wachache bungeni, Bw Junet Mohamed, ambaye ni mwandani mkubwa wa Bw Odinga, aliyedai kwamba ni yeye aliyeshawishi wabunge kuzua fujo bungeni wakati wa kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2018 ulioweka VAT ya asilimia 8 kwa bidhaa za mafuta.
Mswada huo ulikuwa umeungwa mkono na Bw Odinga, ambaye aliwarai wabunge wa ODM kuupigia kura, lakini wengi walimpuuza kinara wao sawa na walivyofanya wenzao wa Jubilee kwa kumpuuza Rais Kenyatta.
Akizungumza katika eneo la Kisauni ambako aliwakabidhi wakazi hatimiliki 3,000 za ardhi, Naibu Rais alisisitiza kwamba Bw Odinga ana sifa ya kuvuruga kila muungano wa kisiasa anaoungana nao.
Kulingana naye, muafaka wa Bw Odinga na Rais Kenyatta ulikuwa bora kwa kuleta amani na utulivu nchini lakini sasa anaona kana kwamba unatumiwa kuvuruga Jubilee na kuafikia kile alichosema ni malengo ya kibinafsi.
Bw Odinga na Rais Kenyatta walikubaliana kufanya kazi pamoja mnamo Februari kufuatia msukosuko uliozuka baada ya uchaguzi wa mwaka jana.
“Salamu haikuwa leseni yako kuleta mgawanyiko, propaganda na utapeli katika chama chetu cha Jubilee. Kama wamekuja kugawanya Jubilee na serikali, tunawaambia kwamba tuko macho na tunajua mipango yenu,” akasema Bw Ruto.
Bw Ruto amekuwa akifanya ziara nyingi eneo la Pwani, ambapo amefanikiwa kupata uungwaji mkono wa viongozi kadhaa wa eneo hilo, wengi wakiwa walichaguliwa kwa tiketi ya ODM
Kwenye hafla ya jana alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa wa Pwani wakiwemo maseneta Juma Wario (Tana River), Christine Zawadi (Maalumu) na wabunge Mohamed Ali (Nyali), Benjamin Tayari (Kinango), Aisha Jumwa (Malindi), Getrude Mbeyu (Kilifi), Michael Kingi (Magarini), Ali Wario (Garsen), Jones Mlolwa (Voi), Ali Sheriff (Lamu Mashariki), Stanley Muthama (Lamu West) na Said Hiribae (Galole).
Na wakati akimshambulia Bw Odinga, viongozi wa ODM walikuwa katika ngome yao Nyanza ambapo walimrukia Bw Ruto kwa jinsi anavyojipigia debe katika ngome za kisiasa za Bw Odinga, na wakamwambia hatafua dafu kumharibia umaarufu kiongozi wao.
Wakiongozwa na Kiongozi wa Wachache katika Seneti, Bw James Orengo, Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na mwenzake wa Embakasi Mashariki Babu Owino, viongozi hao walisema Bw Odinga pekee ndiye kiongozi mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko yanayotamaniwa nchini.
“Ruto na Uhuru wamehudumu kwa kipindi kinachoruhusiwa kikatiba pamoja, kwa hivyo Naibu Rais lazima astaafu pamoja na Bw Kenyatta,” akasema Bw Amollo.
Ripoti ya Mohamed Ahmed, Valentine Obara na Rushdie Oudia