KURUNZI YA PWANI: Fedheha ya Fistula yakosesha wanawake matibabu, ndoa zavunjika

NA STEPHEN ODUOR

WANAWAKE wengi katika jamii za Kaunti ya Tana River wamepoteza ndoa zao baada ya waume zao kukosa kuelewa chanzo cha uvundo wa mkojo unaoibuka kutoka kwao hasa baada ya uzazi.

Kile wasichofahamu ni kuwa wake zao wanaugua Fistula, ambayo imewafanya wengi kutengwa na jamii na kuishia kuishi maisha ya upweke, na yenye fedheha chungu nzima, mbali na gharama wanazokumbana nazo kugharamia matibabu yasiyowasaidia.

Bi Faiza, 27 ameishi kujifunga pampers kwa mwaka wa tatu sasa. Ndoa yake ilisambaratika miaka mitatu iliyopita baada ya mumewe kushindwa kuvumilia harufu wala kuelewa chanzo cha harufu hiyo.

“Baada ya kuzaa mtoto wangu wa kwanza hapa nyumbani, ndio hiyo shida ilianza, sasa nikaona iko tu sawa na sikushughulika sana, nilijua tu nitapona,” alisimulia.

Lakini alivyodhania sivyo kwani hali ile iliendelea miezi kadhaa, kwani pasipo kujua, alijipata keshajiendea haja ndogo ghafla alikoketi.

Alipoamua kueleza wakongwe kijijini kuhusu masaibu yake, hawakumpa suluhisho kamili ila ganga ganga ya kumpa matumaini.

Alishauriwa kutumia maji ya chumvi, dawa za kienyeji, mafuta ya aina mbalimbali kusuluhisha tatizo lake lakini juhudi zote hazikufua dafu wala kuzalisha matumaini, kwani hali ilizidi kuzorota.

Katika kaunti hiyo hiyo, Bi Asha, 22 ameishi kupambana na fistula kwa mwaka wa tano sasa. Mbali na kujipata katika hali hiyo baada ya kujifungua nyumbani, alimpoteza mwanawe.

“Nilipoteza mtoto wangu katika hiyo hali, lakini sikujua kwamba niko na fistula mpaka miezi sita baadaye, ndio nikashuku naugua, “alisimulia.

Miezi minne baadae mume wake aliugua na kuaga dunia. Aliolewa mara tatu, lakini kila mmoja wa wanaume wale walipogundua tatizo lake, na uvundo ulokuwa ukimtoka mwilini, waliingiwa na hasira na kumpa talaka bila kujali.

Fistula ni ugonjwa unaoendelea kuwafedhehesha akina dada hawa na wengine wengi, ila inaonekana hawafahamu wanaweza kupata matibabu bora hospitalini.

Kulingana na Dkt Isack Galgalo, kati ya wanawake kumi wanaoletwa hospitalini kutoka kwa jamii zinazokeketa mabinti wao, sita hupatikana na ugonjwa wa fistula.

Alieleza kuwa hospitali huwatafutia wanawake hao matibabu na kuhakikisha kuwa wamerudia hali yao ya kawaida.

“Tumefanya kadri ya uwezo wetu kuhakikisha kuwa tunawatafuta wanawake hawa na kuwarejesha katika afya nzuri, ila hatuwezi kuwapata wakiwa wamejificha. Ni jukumu lao kujitokeza ndipo tupate kuwaelekeza,” alisema.

Kikundi cha maendeleo ya wanawake wakishrikiana na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Tana River, Bi Rehema Hassan nao wamekuwa wakiendeleza kampeni ya kuwatafuta akina mama hao.

Mwenyekiti wa kikundi cha maendeleo ya wanawake Ralia Hassan anasema kuwa changamoto za usafiri hata hivyo imewafanya kusonga kwa mwendo wa kobe katika kuwatafuta akina mama hao.

Habari zinazohusiana na hii