• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Ruto aahidi wakazi fidia za ardhi

Ruto aahidi wakazi fidia za ardhi

Na KAZUNGU SAMUEL

SERIKALI imewahakikishia wakazi wa eneo la Mwache, Kaunti ya Kwale kwamba watalipwa fidia kabla ya ujenzi wa bwawa la Mwache kujengwa katika eneobunge la Kinango.

Naibu wa Rais Bw William Ruto alitoa hakikisho hilo baada ya hofu kutoka kwa wakazi kwamba huenda mradi huo ukaanza bila yao wao kulipwa fidia licha ya kuwa watapoteza zaidi ya ekari 4,000 za ardhi.

Bw Ruto alikuwa akihutubia wakazi katika shule ya msingi ya Mpirani wakati alipoongoza zoezi la kutoa hati miliki zaidi ya 3,000 kwa wakazi wa lokesheni ya Chigato.

“Ninajua kwamba kumekuwa na hofu kuhusu mradi huu na watu wanaona kwamba huenda hawatafidiwa. Serikali hii inafanya kazi kulingana na sheria za Kenya na hivyo basi hakuna mtu hata mmoja ambaye hatalipwa. Kila mtu atalipwa ridhaa kabla ya mradi huu kuanza,” akatoa hakikisho hilo.

Alikuwa ameandamana na Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, pamoja na wanasiasa wengine kutoka ukanda wa Pwani. Waziri wa maji na usafi Bw Simon Chelagui pia alikuwepo.

Gavana Mvurya alikuwa amedai awali kwamba kulikuwa na propaganda nyingi ambazo zinaendelea kuhusiana na fidia kwa wakazi, jambo ambalo lilikuwa limeanza kuzua taharuki.

“Kuna watu hata walikuwa wameanza kutangaza kwamba mimi nimelipwa tayari pesa kwa ajili ya mradi huu. Hiyo sio kweli na ninataka hili liwe wazi. Fidia ikija italenga tu wale ambao wataathiriwa na mradi huu wa Mwache,” akasema Bw Mvurya.

Mbunge wa Kinango Bw Benjamin Tayari alimtaka naibu wa rais pamoja na waziri wa maji kuhakikisha kwamba wakazi wanapatiwa asilimia kubwa ya ajira wakati mradi huo ukianza.

“Tunataka waziri ujue kwamba vijana wetu hawana ajira na tungeomba kwamba pindi tu kazi ikianza, basi wawe watu wa kwanza kupata nafasi za ajira, kasha wengine wafuate baadaye,” akasema Bw Tayari.

Tayari serikali kuu imetenga jumla ya Sh1.4 billioni kama fidia kwa zaidi ya wakazi 3,000 ambao watapoteza ardhi kwa kutoa nafasi ya ujenzi wa bwawa hilo.

Waziri Chelagui alisema kuwa maji yatakayotolewa katika bwawa hilo yatasaidia kumaliza shida ya maji katika kaunti za Mombasa na Kwale.

“Bwawa hili litakuwa na uwezo wa kutoa lita 186,000 za maji na katika hili, asimilia 30 ya maji haya yatakuwa yakitumika katika kaunti ya Kwale na asimilia 70 ifike katika kaunti ya Mombasa. Mradi huu ni muhimu sana na tutahakisha kwamba unatekelezwa vizuri kwa faida za kila mkenya,” akasema Waziri Chelagui.

Kulingana na Bw Ruto, mradi huo utagharimu takribani Sh30 bilioni ingawa awamu ya kwanza ni ya ujenzi wa bwawa hilo ambao utagharimu Sh14.8 billioni.

“Kutakuwa na miradi mingi ambayo inahusiana na mradi huu ambayo itagharimu mamilioni ya fedha lakini ambayo vile vile itatumika kuimarisha miradi ya wananchi wa kaunti ya Kwale,” akasema Bw Ruto.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Fedheha ya Fistula yakosesha wanawake...

TAHARIRI: Wadau watatue shida za vijana

adminleo