Wabunge wakerwa na ziara za Amina Mohamed mitihani ya KCPE na KCSE ikikaribia
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wamekerwa na hatua ya Waziri wa Elimu Amina Mohamed kufanya ziara nyingi za kigeni wakati huu ambapo wanafunzi wa darasa la nane na wale wa kidato cha nne wanajiandaa kwa mitihani ya kitaifa.
Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu Jumanne waligadhabika pale Waziri Mohamed alipofeli kufika mbele yao kutoa maelezo kuhusu hatima ya watahiniwa kutoka maeneo yanayoshuhudia vita katika kaunti za Narok na Nakuru.
Katibu wa Wizara hiyo Belio Kipsang’ na Waziri Msaidizi Simon Kachapin pia hawakufika mbele ya kamati hiyo kumwakilisha bosi wao ambao inasemekana kuwa yuko katika ziara ya kikazi katika mataifa ya nje.
Barua iliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo ilisema kuwa Dkt Mohamed atarejea nchini mnamo Oktoba 18, siku chache kabla ya kuanza kuwa mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE).
“Hatujafurahishwa na jinsi Waziri wa Elimu na Katibu wake wanavyoendesha wizara hii muhimu. Wameacha shughuli muhimu kama mitihani kushughulikiwa na maafisa wa ngazi za chini. Na tunapowahitaji hawapatikani,” akalalamika mwenyekiti wa Kamati hiyo Julius Melly.
Naye Mbunge wa Malava Malulu Injendi alisema Wiziri huyo hakupaswa kusafiri nje wakati huu ambapo wanafunzi wanajiandaa kwa mitahani ya kitaifa kw sababu anahitajika kukagua shughuli zote za maandilizi kuhakikisha kuwa zinaendeshwa zilivyopangwa.
“Bi Amina anapas kufahamu kwamba yeye sio waziri wa mashauri ya kigeni bali anasimamia Wizara muhimu ya Elimu,” Bw Injendi akaongeza.
Naye Mbunge wa Kilome Mhandisi Thaddeus Nzambia alisema kuwa mchakato kuandaliwa kwa mtaala mpya hauendeshwi vizuri kwa ajili ya uzinduzi wa mfumo mpya wa elimu hapo mwakani.
“Tunakerwa na utendakazi wa Taasisi ya Utayarishaji Mitaala Nchini (KICD) kwa kwa sababu kufikia sasa walimu wengi hawafahamu ikiwa majaribio ya mtaala mpya yatafanyika,” akasema Bw Nzambia.
Vile vile, Mbunge huyo alikerwa na hatua ya taasisi hiyo kusambaza vitabu shuleni katika muhula huu wa tatu, siku chache kabla ya watahiniwa kuanza mitihani ya kitaifa.
“Kuna haja gani kwa KICD kuaza kusambaza vitabu wakati huu ilhali zimesalia siku chache kabla ya mitihani ya KCPE na KCSE kuanza. Je, wanafunzi hao watafaidi vipi kutokana na vitabu hivyo?” akauliza Mbunge huyo wa chama cha Wiper.
Bw Melly alimshauri Dkt Amina kuiga mfano wa mtangulizi wake, Dkt Fred Matiang’i ambaye alikuwa akizuri shule mbalimbali kila mara haswa mitihani ilipokuwa ikikaribia.