• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 5:41 PM
Kidero apinga kushtakiwa upya

Kidero apinga kushtakiwa upya

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya  Nairobi Dkt Evans Kidero Alhamisi aliomba mahakama kuu ifutilie mbali hatua ya kufunguliwa mashtaka mapya na tume ya kupambana na ufisadi (EACC) baada ya kuvamia makazi yake wiki mbili zilizopita.

Dkt Kidero alilia hoi kuwa, “endapo maafisa wa EACC hawatazuiliwa kukandamiza haki za  wananchi na kuzikaidi basi nchi hii hakuna mtu atakayemiliki mali.”

Wakili wa Dkt Kidero, Profesa Tom Ojienda (pichani) alitoana jasho na mawakili kutoka EACC, afisi ya mwanasheria mkuu, afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) na afisi ya uchunguzi wa jinai (DCI) alipowatahadharisha kuwa , “mapambano yatakuwa makali.”

Prof Ojienda aliambia mahakama kuwa , wakati umewadia korti , isimame kidete na kutetea haki za wananchi wanaodhulumiwa na maajenti wa Serikali.

“Nataka nipewe fursa nionane na hawa maajenti wa Serikali wasioheshimu haki za wananchi kwa mujibu wa katiba,” alisema Prof Ojienda , akimtazama wakili Wesley Nyamache anayewakilisha DPP akiwa na Bi Anne Pertet na Bi Ruth Mwila.

“Naomba hii mahakama inikinge dhidi ya Prof Ojienda. Mbona anaongea akinitazama? Nahisi kile kinginge nitapata ni kuzabwa kofi,” alidokeza Bw Nyamache.

Prof Ojienda alisema hana husuda wala chuki dhidi ya mawakili wa DPP , DCI ,EACC na AG ila atahoji vikali tabia ya maajenti wa Serikali kuvamia makazi ya Dkt Kidero na kutwaa hati zake kinyume cha sheria.

Anaomba maagizo yatolewe asishtakiwe na hati zilizotwaliwa zote arudishiwe.

“Endapo hii mahakama haitakomesha tabia ya maafisa wa EACC na vitengo vingine vya  Serikali vya upelelezi kuvamia makazi na afisi za wananchi na kutwaa hati basi itakuwa vigumu mmoja kumiliki mali humu nchini,” wakili Prof Tom Ojienda anayemtetea Dkt Kidero alimweleza Jaji Hedwig Ong’udi.

Prof Ojienda aliomba mahakama  imkubalie mlalamishi awasilishe ushahidi kuthibitisha jinsi haki zake zilivyokandamizwa baada ya maafisa wa EACC kuvamia makazi yake na kutwaa stakabadhi muhimu.

“Naomba hii mahakama inipe fursa nieleze jinsi haki za Gavana huyu wa kwanaza Nairobi zimekiukwa,” alisema Prof Ojienda alisema  akiongeza , “ Nataka nikutane na maajenti wa EACC , maafisa katika afisi ya mkurugenzi wa jinai (DCI) na mkurugenzi wa mashtaka ya umma.

You can share this post!

Wakenya washauriwa kuchukua bima ya mazishi

Mabwanyenye waongezeka kwa kasi nchini licha ya uchumi...

adminleo