• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Rais achemkia NCPB kwa kukosa kulipa wakulima

Rais achemkia NCPB kwa kukosa kulipa wakulima

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta ameonyesha kuguswa na kero la maelfu ya wakulima wa mahindi ambao wamecheleweshewa malipo ya mazao yao.

Akizungumza kwa ukali na uchungu Alhamisi kwenye Maonyesho ya Kilimo ya Nairobi, Rais Kenyatta alisema serikali iliwatengea wakulima pesa kwenye bajeti ya mwaka uliopita, lakini maafisa wa Bodi ya Nafaka (NCPB) wakaamua kuwalipa wafanyabiashara badala ya wakulima.

“Lazima ukweli usemwe. Pesa za kulipa wakulima wa mahindi zilikuwa kwenye bajeti ya mwaka uliopita. Watu wa NCPB badala ya kulipa wakulima halisi walianza kulipa matajiri wafanyabiashara na kumalizia pesa, badala ya kulipa mkulima yule ametoa jasho,” Rais akasema.

Akiapa kwa jina la Mungu, Rais aliwaambia maafisa wa bodi hiyo kudhubutu kitendo cha aina hiyo tena.

“Nawahakikishia na ninaapa mbele ya Mungu, jaribuni hivyo tena na mtaona kitakachowatendekea. Sisi hatutaki mchezo tena kwa sababu tumeona yale ambayo mumefanya na wale ambao walifanya tutawafuata. Pesa ya serikali ni ya mwananchi, kwanza lipa mwananchi yule ambaye ametoa jasho ya kulima shamba lake,” akasema.

Wakulima hao walianza kulipwa Alhamisi, japo baada ya kulalamika mara nyingi na hata viongozi haswa wa kutoka North Rift kutishia kuongoza maandamano ya kusukuma wakulima kulipwa.

Rais Kenyatta jana alisema kilimo cha mahindi kimezidi kunawiri, akisema mavuno ya zao hilo mwaka huu yamepanda hadi magunia milioni 41, ikilinganishwa na magunia milioni 34 mwaka uliopita, huku mavuno mengine zaidi yakizidi kutarajiwa.

“Mabadiliko tuliyofanya yameanza kuzaa matunda. Kutokana na upanzi wa msimu wa mvua fupi vilevile, tutaweza kupata magunia milioni sita zaidi, ikiashiria mwaka huu tutazalisha jumla ya magunia milioni 47,” akasema.

Aliongeza kuwa ikizingatiwa kuwa hadi sasa bado kuna magunia milioni 9.8 kwenye hifadhi, hiyo itamaanisha kuwa mwaka huu kutakuwa na magunia 56milioni, kiwango cha juu ikilinganishwa na kiwango linalotumia taifa kila mwaka cha magunia milioni 52.

You can share this post!

Wakulima wa majani chai kuvuna pesa za kihistoria

Waziri aiomba radhi jamii ya Abasuba watoto wao kusomeshwa...

adminleo