Obado Mkenya wa kwanza kushtakiwa kwa mauaji ya mtoto asiyezaliwa
Na Richard Munguti
GAVANA wa Migori, Okoth Obado na washukiwa wengine wawili ndio wa kwanza katika historia ya Kenya kushtakiwa kwa mauaji ya mtoto ambaye hajazaliwa.
Bw Obado, aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori, Caspal Obiero walikanusha mashtaka mawili ya kumuua Baby Sharon na Sharon Otieno mnamo Septemba 3, 2018 katika eneo la Owade, Kaunti ya Homabay.
Gavana Obado ataendelea kukaa katika rumande hadi Ijumaa wiki hii atakapowasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana.
Ombi lake la kwanza lilikataliwa na jaji Jessie Lesiit wiki mbili zilizopita.
Alipokuwa akiwasilisha ombi la kushtakiwa kwa watatu hao kwa mauaji ya Baby Sharon, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Alexander Muteti alimweleza Jaji Jessie Lesiit kuwa maisha ya binadamu huanza punde tu mimba inapotungwa.
Bw Muteti alisema kushtakiwa kwa watatu hao kwa mauaji ya Baby Sharon na mama yake kutatia kikomo mijadala ya miaka mingi kuhusu ikiwa kijusi ni binadamu anayeweza kuuawa.
Jaji Lesiit ameombwa na mama yake marehemu Sharon, Bi Melida Auma Otieno awanyime dhamana washtakiwa akisema kuachiliwa kwao kutahujumu haki na maslahi ya umma.
Kwenye nakala ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani jana, Bi Otieno amesema kuwa familia yake inaishi kwa hofu kutokana na vitisho ambavyo wamepokea mara kwa mara kufuatia kushikwa kwa Bw Obado na wenzake.
“Mtu mmoja wa familia aliponyoka alipokuwa ametekwa nyara na watu watano siku ile mwiili wa Sharon ulipofanyiwa upasuaji,” alidokeza Bi Otieno.
Mama huyo amesema kuwa yeye na watu wa familia yake wamekuwa wakiishi kwa hofu na kwamba kuachiliwa kwa washtakiwa hao watatu kutahatarisha maisha yao.
Aliongeza kuwa amekuwa akitukanwa na kutishwa na watu wanaofika mahakamani kila wakati kesi dhidi ya Bw Obado inapowasilishwa.
“Familia yangu inaishi kwa hofu. Ikiwa washtakiwa hawa wataachiliwa kwa dhamana kuna hatari,” akasema Bi Otieno.
Mahakama pia imejulishwa kuwa kuwaachilia watatu hao kwa dhamana kutawafanya mashahidi waishi kwa hofu na kutishwa.
Wakti huo huo, shirika la kutetea haki za wanawake (FIDA) liliwasilisha ombi la kutaka likubaliwe kushiriki katika kesi hiyo.