Juhudi za Naibu DPP kuhusu kesi ya Mwilu zaambulia pakavu
Na RICHARD MUNGUTI
JARIBIO la naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bi Dorcus Oduor la kutaka agizo linalozuia kushtakiwa kwa Naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu liondolewe limegonga mwamba.
Bi Oduor alisema muda ambao agizo lililotolewa na Jaji Enoch Mwita uliyoyoma na “hakuna agizo linalomzuia DPP akimshtaki DCJ Mwilu na wakili Stanley Kiima kwa ufisadi.”
Ombi hilo la Bi Oduor liliwazuzua wengi hata wakati mmoja Jaji Mwita akamwuliza , “wewe unataka kesi ipi iendelee?”
Jaji Mwita alimweleza Bi Oduor kwamba katika kesi moja DPP anataka jopo la majaji watatu wateuliwe kuamua kesi ya DCJ Mwilu , lingine ni kesi hiyo ipelekwe mbele ya kitengo cha mahakama kuu cha kuamua kesi za ufisadi na ombi la kufutiliwa mbali kwa agizo linalozima DPP akimshtaki DCJ.
“Amua kesi unayotaka hii mahakama iamue,” Jaji Mwita.
Swali hilo lilimduwaza Bi Oduor hata akaanza kutapatapa.
Lakini mawakili James Orengo, Dkt John Khaminwa na Daniel Maanzo walipinga hatua ya Bi Oduor wakisema, “ombi la kusitisha kushtakiwa kwa DCJ Mwilu litaendelea kuwako hadi mahakama kuu itakapoamua ikiwa DPP alifuata sheria kumfungulia mashtaka jaji huyu wa pili kwa ukuu nchini.”
Jaji Mwita alitupilia mbali ombi la Bi Oduor na kumzuia DPP akimshtaki DCJ.