UHURU: Wakenya hawana haja na siasa za 2022
Na CHARLES WASONGA
Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa aliwahimiza viongozi wa kisiasa kusitisha siasa za 2022na badala yake kutekeleza yale waliyowaahidi Wakenya katika manifesto za vyama vyao wakati wa uchaguzi uliopita.
Rais alisema kwa sasa, Mkenya wa kawaida hana haja ya siasa za mwaka wa 2022 bali anajali zaidi hatua wanazochukua viongozi kuboresha maisha yao.
“Huu si wakati wa kuzungumzia uchaguzi wa mwaka wa 2022. Kwa sasa jambo hilo si muhimu kwa Wakenya wa kawaida,” akasema Rais Kenyatta.
“Wakenya wanataka kujua ni nini tunafanya leo, kesho, wiki ijayo na mwezi ujao kuhakikisha wanapata chakula cha kila siku; wanapata huduma za afya kwa gharama ya chini; na wana nyumba zifaazo. Mwisho wa siku, hayo ndiyo muhimu kwa Wakenya, si siasa,” Rais Kenyatta akaeleza.
Rais Kenyatta alisema haya leo katika Chuo cha Mafunzi ya Uanuwai cha Meru alipohutubia Kongamano la Saba la Tume za Kikatiba na Afisi Huru.
Rais alisema mipango inayotekelezwa na serikali yake inatokana na maoni ya wananchi, ambapo wanahusishwa katika maamuzi moja kwa moja, huku wakipewa uhuru wa kusema wanayohitaji serikali yao kuwatendea.
“Mwaka jana, nilibahatika kuwasiliana moja kwa moja na wananchi wa kawaida – wake kwa waume, vijana na watu wasiojiweza – kote nchini. Nilisikia mahitaji yao, matarajio yao, na pia malalamishi yao kuhusu awamu yangu ya kwanza uongozini,” akasema Rais Kenyatta.
Alisema ni kutokana na kutangamana na wananchi na kusikiza maoni yao ndipo alibuni wazo la Agenda Nne za Kuu za Maendeleo, ambazo zinahusu ujenzi wa nyumba bora za gharama ya chini, utoaji huduma bora za afya kwa wote, lishe bora, na kubuni nafasi za kazi kipitia ustawishaji wa viwanda.
“Maono yangu kuhusu Kenya yalitokana na kuhusishwa kwa wananchi na yanazingatia maoni ya Wakenya. Hasa, maono hayo si yangu bali ni ya mamilioni ya Wakenya. Kuhusishwa kwa umma – kama nilivyopendekeza kwenu zaidi ya mara moja – hufanya kazi,” akasema Rais Kenyatta.
Kiongozi wa taifa alitoa wito kwa tume za kikatiba kutekeleza majukumu yao, akiongeza kwamba kuna visa ambapo tume hizo zimezembea katika kutekelezaji wa wajibu wao huku zikitumia uhuru wao kama kinga ya kuzuia kuchunguzwa.
“Hakikisho la kuendelea kuhudumu wakati mwengine limetumiwa kama ngao ya kujikinga kutokana na uwajibikaji na utekelezaji wa sheria; uhuru huo umechukuliwa kimakosa kumaanisha kujitenga na serikali, akasema Rais Kenyatta.
Rais alizihimiza tume hizo kuzingatia uwazi na kuruhusu kuchunguzwa kupitia kuhusishwa kwa umma.
“Kushauriana na Wakenya si jambo la hiari, hili ni jambo la lazima kikatiba katika ufanisi wa uongozi,” akasema Rais Kenyatta.
Rais alitoa wito kwa tume hizo, ambazo zote zimebuniwa kupitia pendekezo la kifungu cha 15 cha Katiba, kuzingatia viwango vya juu vya utendakazi zinapohudumia Wakenya.
“Ningependa kuwashauri Wakenya wote watumie nafasi zilizoko za ushirikishi serikalini na kwa ustaarabu kuitisha huduma bora kutoka kwa taasisi zote za serikali. Hiyo ni haki yenu,” akashauri kiongozi wa taifa.