Habari Mseto

Athari za HIV Bungoma kupigwa darubini

October 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la kuchunguza athari za kuenea kwa virusi vya HIV nchini Kenya (KENPHIA) litaendesha uchunguzi katika nyumba 500 katika kaunti ya Bungoma.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa uchunguzi huo katika uwanja wa Chuo cha Mafunzi ya Matibabu (KMTC) Bungoma  Dkt Thanitius Ochieng kutoka kitengo cha Wizara ya Afya kinachohusika na uhamasishaji alisema zoezi hilo linaendeshwa kwa lengo la kubaini athari za kuenea kwa virusi vya HIV na ugonjwa wa ukimwi katika kaunti hiyo.

Dkt Ochieng’ alisema wahudumu wa KENPHIA watawapima watu kujua hali yao Ukimwi huku walengwa wakiwa ni wale walio na umri wa hadi miaka 64.

Alisema kando na HIV wahudumu hao pia wanaendesha uchunguzi kuhusu maradhi ya Hepatitis B, kisonono pamoja na kukagua hali ya afya ya kina mama waja wazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Dkt Ochieng’ alitoa wito kwa jamii za eneo hilo kuunga mkono mpango huo akisema usiri wa wahusika utadumishwa katika zoezi hilo na kwamba hakuna atakayelazimisha kupimwa.