• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Rais kuelezea mbinu za kufufua sekta ya sukari nchini

Rais kuelezea mbinu za kufufua sekta ya sukari nchini

Na LEONARD ONYANGO

KUPOROMOKA kwa viwanda vya sukari katika maeneo ya Magharibi ni miongoni mwa masuala makuu ambayo Rais Uhuru Kenyatta atayazungumzia wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Mashujaa hapo Jumamosi ijayo katika uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega.

Msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena jana alisema Rais Kenyatta ataangazia mikakati ya uboreshaji uzalishaji wa viwanda vya sukari hasa vya Nzoia na Mumias.

Bi Dena alisema hayo wiki moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na baadhi ya viongozi wa Magharibi katika Ikulu ya Nairobi walioongozwa na waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho katika Ikulu ni Magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Sospeter Ojaamong (Busia), Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Wilberforce Otichilo (Vihiga) na Wycliffe Wangamati (Bungoma).

Wengine ni maseneta Moses Wetang’ula, (Bungoma), Amos Wako (Busia), Cleophas Malala (Kakamega), George Khaniri (Vihiga) na Michael Mbito (Trans Nzoia.

“Katika kikao hicho masuala ya sukari na mahindi yalipewa kipaumbele. Kuhusu viwanda vya miwa na sekta nzima ya sukari, Rais Kenyatta alilipa jopo linaloshughulikia suala hilo makataa ya mwezi mmoja kukamilisha ripoti yake,” akasema Bi Dena.

“Hili ni suala ambalo rais atalizungumzia kwa kina kwenye sherehe ya Mashujaa mjini Kakamega wikendi ijayo,” akaongezea.

Wakati huo huo, Bi Dena alisema kuwa ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York nchini Amerika zitaanza safari zake Oktoba 28.

“Rais Kenyatta kwa ushirikiano na Shirika la Ndege la Kenya watawatunuku vijana wawili wa Kenya waliobobea kwenye nyanja tofauti tiketi za kusafiri kwenye ndege hiyo moja kwa moja kutoka Kenya hadi Amerika,” akasema.

Bi Dena pia alieleza kuwa Rais wa Namibia Hage Geingob anatarajiwa kuzuru Kenya Ijumaa hii kwa ziara rasmi ya kiserikali.

Alisema akiwa nchini, Rais Geingob atashauriana na Rais Kenyatta.

You can share this post!

Familia ya Sharon yakejeli wanaodai mazishi yatagharimu...

Referenda ni nafasi murua kwa wanawake kutetea jinsia...

adminleo