• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Magavana wa Magharibi kushirikiana kibiashara

Magavana wa Magharibi kushirikiana kibiashara

Na DENNIS LUBANGA

MAGAVANA wa kaunti tano za eneo la Magharibi wamekubaliana kushirikiana ili kuboresha biashara na uwekezaji katika eneo hilo.

Kulingana nao, hatua hiyo imetokana na kuwa kaunti hizo zinakumbwa na changamoto zinazofanana kama vile ukosefu wa mashirika ya kutosha ya kifedha, kuangamia kwa viwanda muhimu vya kilimo miongoni mwa zingine.

Makubaliano hayo ya kibiashara yalifanywa Ijumaa katika kaunti ya Bungoma kwenye mkutano ulioandaliwa na Gavana Wycliffe Wangamati.

Wenzake wanne ni magavana Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Wilberforce Otichillo (Vihiga), Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Sospeter Ojaamong (Busia).

Bw Oparanya alisema wataanza kwa kutoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo kwani ndiyo inayohusu kaunti hizo zote, hasa kilimo cha miwa na mahindi.

“Tumefanya uchanganuzi wa uchumi wetu na tumetambua kuwa tunategemea sana mahindi na miwa. Lakini kama mjuavyo, kilimo cha miwa kimedorora sana na cha mahindi kwa sasa kinaelekea pabaya. Tunatafuta jinsi ya kutatua changamoto hizi,” akasema Bw Oparanya.

Alifichua wamekuwa wakikutana na wadau mbalimbali katika sekta ya sukari na mahindi ili kuboresha faida za kiuchumi kutokana na sekta hizo.

“Hatutaki kushughulikia masuala mengi kwa wakati mmoja na kukosa mafanikio. Kwa sasa tunashughulikia haya mawili na mengine yatafuata,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Wangamati alisema inahitajika kuwe na mfumo mmoja wa utozaji ushuru na mfumo huo utumike katika kila kaunti ili kuimarisha kasi ya maendeleo katika eneo hilo.

“Kwa mfano, kama wewe ni mhudumu wa matati kati ya Bungoma na Kakamega, haifai ulipishwe ada za kibandiko tofauti katika kila kaunti. Hivi tutavutia biashara baina ya kaunti zetu,” akasema.

You can share this post!

DPP ataka mnajisi aozee jela maisha sio miaka 20

TAHARIRI: Tulinde watoto dhidi ya maovu

adminleo