Kimataifa

Museveni awaomba Waganda msamaha

October 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Leonard Mukooli

RAIS Yoweri Museveni ameomba msamaha kwa niaba ya serikali yake kwa wakazi wa Kaunti Ndogo ya Bukalasi, Wilaya ya Bududa ambapo watu zaidi ya 40 walifariki kwenye maporomoko ya ardhi Alhamisi iliyopita.

Museveni aliomba msamaha kwa jinsi serikali ilivyokosa kuwahamisha wakazi wa eneo hilo na kuwapa ardhi katika maeneo mengine salama kwa wakati ufaao.

Kulingana naye, mpango wa kuwahamisha uliingizwa siasa na kufanya ucheleweshwe lakini suala hilo sasa limetatuliwa.

“Kama siasa hazingeingizwa, basi watu wangekuwa wamehamishwa hadi katika maeneo mengine kwa zamu,” akasema alipozuru eneo hilo Jumapili.

Aliandamana na maafisa wengine wakuu wa serikali akiwemo Waziri Mkuu Ruhakana Rugunda.

Ziara yake ilitokea saa chache baada ya serikali kupeleka bidhaa za kusaidia waathiriwa wa mkasa huo.

Bidhaa zilizopelekwa ni pamoja na vyakula, hema, blanketi, mitungi ya maji, vyombo vya kupikia, beseni, sahani, neti za kuzuia mbu, vikombe na nyinginezo.

Mkasa huo uliathiri zaidi wakazi wa eneo la Bukalasi ambako huwa kuna hatari ya maporomoko ya ardhi wakati mvua kubwa inaponyesha.