Ripoti ya mabilioni ya madeni yanyima Gavana Kinyanjui lepe la usingizi
Na FRANCIS MUREITHI
Kwa Muhtasari:
- Imebainika kuwa deni la Sh722 milioni pekee ndilo halali kati ya deni la Sh3 bilioni ambalo Gavana Kinyanjui alilirithi
- Mengi ya madeni ambayo serikali ya kaunti inadaiwa yaliidhinishwa katika kipindi cha mwisho cha mwaka 2017 miezi michache tu kabla ya uchaguzi mkuu
- Hata hivyo, Gavana Kinyanjui amewahakishia wanakandarsi waliofanya kazi safi watalipwa madeni yao bila kucheleweshwa
- Idara kadha zilipatikana na makosa ya kununua bidhaa kwa kuongeza bei
WAKATI muhula wa kwanza wa Gavana Lee Kinyanjui wa Kaunti ya Nakuru ukiingia hatua muhimu, huenda kipindi chake cha kwanza kikakumbwa na mgogoro wa malimbikizi ya madeni.
Kulingana na ripoti ya mkaguzi wa hesabu wa ndani, imebainika kuwa ni deni la Sh722 milioni pekee ndilo halali kati ya deni la Sh3 bilioni ambalo Gavana Kinyanjui alilirithi kutoka kwa Gavana Kinuthia Mbugua
Deni hilo linawakilisha asilimia 24 ya madeni yote yaliosalia.
Sasa inamaanisha kuwa deni la zaidi ya Sh2 bilioni ni feki kwani hazina stakabadhi za kudhibitisha kuwa wanakandarasi walitoa huduma kwa kaunti katika kipindi cha makadirio ya fedha cha mwaka wa 2016 /2017.
Aidha ripoti hiyo imefichua kuwa zaidi ya Sh300 milioni hazijulikani jinsi zilivyoingizwa kwenye hesabu ya madeni ya kaunti ilhali hakuna kandarasi zilizotolewa.
Kufilisisha kaunti
La kustaajabisha ni kuwa mengi ya madeni ambayo serikali ya kaunti inadaiwa yaliidhinishwa katika kipindi cha mwisho cha mwaka 2017 miezi michache tu kabla ya uchaguzi mkuu.
Kati ya idara ambazo zinadaiwa kupunja pesa za umma ni pamoja na idara ya mazingira, maji na mali ya asili na idara ya barabara.
Ripoti hiyo inawashuku wafanyakazi wa kaunti kwa kushirikiana na matapeli kufilisisha kaunti kwa njia ya udanganyifu.
Gavana Kinyanjui sasa amewaalika maafisa wa kupambana na ufisadi na maadili kuchunguza baadhi ya wafanya kazi hao.
“Huu ni wizi wa mchana wa mali ya umma na ni lazima wafanyakazi waliohusika na ufisadi huu wachunguzwe na wakipatikana na hatia washtakiwe kulingana na sheria za nchi kwani sitakubali kuongoza kaunti iliyojaa wafanyakazi wafisadi
Aidha, Gavana Kinyanjui alisema kuwa lazima atimize ahadi yake kwa zaidi ya wakazi milioni mbili wa kaunti ya Nakuru.
Bw Kinyanjui alisema kuwa baadhi ya miradi haikuwa kwenye bajeti huku zabuni zilizotolewa zikiwa hazina stakabadhi muhimu.
Kukithiri kwa ufisadi
“Ni jambo la kuhuzunisha kuwa kaunti inaonekana kana kwamba ina deni la mabilioni ilhali ripoti ya mkaguzi wa hesabu imefichua kuwa zabuni nyingi zilikuwa na ufisadi mwingi,” akasema Bw Kinyanjui.
Hata hivyo, Gavana Kinyanjui amewahakishia wanakandarsi waliofanya kazi safi watalipwa madeni yao bila kucheleweshwa tena.
Ripoti hiyo ya kurasa 700, imefichua kuwa sheria za kukabiliana na wizi wa pesa za umma katika kaunti zina kasoro nyingi kwani zimewapa wafanyakazi wafisadi mwanya wa kupora pesa za umma.
Ripoti hiyo ambayo imezua wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi katika kaunti hii ilitayarishwa kati ya Oktoba na Disemba mwaka 2017 na tayari imekabidhiwa Gavana Kinyanjui.
Hata hivyo, wakazi wa Nakuru wanasubiri kwa hamu na ghamu ikiwa Gavana Kinyanjui atatekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo kwa kina.
Huenda deni lisilipwe
Kwa mfano deni la Sh656milioni huenda lisilipwe kwa vile hakuna rekodi za kudhibitisha kuwa kazi ilifanyika huku Sh523 milioni zingine zikiwa na kasoro ya stakabadhi.
Hali kadhalika deni la Sh9million katika idara kadha zilipatikana na mushkili kwani stakabadhi hazikuwa sahihi kulinga na sheria za zabuni.
Idara kadha zilipatikana na makosa ya kununua bidhaa kwa kuongeza bei hizo kupita kiasi cha bei zilizotengwa na kuidhinishwa. Idara nyingine iliyokumbwa na ufujaji wa pesa za umma ni idara ya elimu ambapo ripoti hiyo ilifichua kuwa deni la Sh14 milioni limekuwepo tangu mwaka wa 2014.
Idara ya Mazingira, Maji na mali ya Asili hali kadhalika ilipatikana na doa la kuongeza deni kwa zaidi ya Sh14 milioni ilhali idara ya Ardhi ilipatikana na kasoro ya kuongeza deni kwa Sh2.3 milioni.