Jopo lateuliwa kupima mamlaka ya DPP
Na RICHARD MUNGUTI
KATIKA historia ya nchi hii hakuna jaji amewahi kamatwa na kushtakiwa kabla ya kuhojiwa na tume ya kuajiri idara ya mahakama (JSC).
Kesi ya Naibu Jaji Mkuu (DCJ) Mwilu ndiyo ya kwanza kuwahi kufanyika tangu nchi hii ianze kujitawala miaka 55 iliyopita.
Kitendo hiki cha kumtoa DCJ Mwilu ofisini na kumpeleka kortini kimeleta mkinzano mkali kati ya afisi ya raia na idara ya mahakama.
Ndipo mbivu na mbichi zijulikana mamlaka ya utenda kazi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Noordin Haji yamehojiwa na DCJ Mwilu.
DCJ Mwilu anaomba mahakama kuu itafsiri Kifungu nambari 157 cha Katiba kinachompa mamlaka DPP uwezo wa kumfungulia mshukiwa yeyote mashtaka ikiwa amevunja sheria.
Huku akinusa kuwa huenda dau lake likaenda mrama DPP aliwasilisha ombi jopo la majaji zaidi ya mmoja iteuliwe kuamua ikiwa alitumia mamlaka yake vibayana kumshtaki DCJ Mwilu.
DPP anaomba korti iamue iwapo kitendo cha kumshtaki DCJ Ngilu kinagonganisha afisi ya Rais na Idara ya Mahakama.
Afisi ya DPP iko chini ya afisi ya Rais pamoja na afisi ya Mwanasheria mkuu (AG).
DCJ Mwilu, kwa upande wake anasema haki zake binafsi zimekiukwa na kuongeza kuwa idara yote ya mahakama inakabiliwa na tisho la kuvurungwa na afisi ya rais.
Kuamua mtafaruku huu Jaji Mkuu (CJ) David Maraga atateua jopo la majaji watatu kusikiza kesi na kubaini ikiwa Bw Haji alitumia vibaya mamlaka ya kwa kunyoosha mkono na kumkamata DCJ Mwilu akiwa katika harakati za kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
DCJ Mwilu amehoji kitendo cha Bw Haji kumkamata na kumfikisha kortini kujibu mashtaka akiwa angali naibu wa CJ na wapili kwa ukuu katika idara ya Mahakama.
Watakapotoa uamuzi iwapo Jaji anayehudumu anaweza kamatwa kiholela na kusukumwa kortini akiwa angali anahudumu.
Swali ambalo jopo la majaji watatu watakalojibu ni ikiwa afisi ya rais inaweza dhulumu idara ya mahakama ambayo ni mojawapo wa vitengo vitatu vinavyojumuisha Serikali.
“Je DPP anahujumu uhuru wa idara ya mahakama na kukaidi sheria zinazoithibiti? ” anahoji DCJ Mwilu.
Katika ushahidi aliowasilisha mahakamani , DCJ Mwilu anasema DPP amekaidi sheria zote kwa kuvuka mipaka na kutwaa mamlaka ya tume ya kuajiri wafanyakazi wa idara ya mahakama (JSC) iliyopewa mamlaka ya kuwaadhibu majaji na mahakimu wanaojihusisha na visa visivyoambatana na mwongozo wa idara ya mahakama.
Kwa mujibu wa sheria JSC ndiyo hupokea malalamishi dhidi ya majaji na mahakimu kisha inawahoji na kutoa maamuzi iwapo wako na makossa au la.
DCJ Mwilu anasema iwapo kuna yeyote aliyedai alikosa ama kukiuka maadili ya kazi ya ujaji , basi angelipeleka malalamiko kwa JSC kisha achunguzwe na ripoti kutolewa kwa Rais Uhuru Kenyatta ateue jopo la kuamua kesi dhidi yake.
Baada ya jopo hilo la rais kutoa uamuzi humpendekezea kinara wa nchi amtimue kazini ama achukuliwe hatua za kisheria.
DCJ Mwilu amesema kupitia kwa mawakili wanaomwakilisha kuwa DPP amekiuka sheria na mwongozo unaofuatwa kumwondoa jaji wanaolindwa kikatiba dhidi ya kutimuliwa ofisini kama makanga.
Jopo atakaloteua CJ litakuwa na kibarua kigumu kwa vile kitaamua iwapo mmoja akipokea mkopo wa Benki na aulipe , makosa ni yapi?
Je ni uhalifu upi mmoja utenda akikopa pesa kutoka kwa benki?
Swali lingine ambalo DCJ Mwilu anauliza ni ikiwa benki iliyomkopesha pesa haijalalamika kwa nini DPP amempeleka mahakamani kumdhulumu.
Pia DCJ Mwilu anahoji ikiwa mahakama ikitoa uamuzi wa kesi waliosikiza na kuamua wanapasa kushtakiwa?
Swali lingine ambalo mawakili Okong’o Omogen, James Orengo, Daniel Maanzo na wengine wasiopungua 1,000 kutoka kwa shirika la wanawake mawakili (FIDA) ni je kuna mtafaruku kati ya afisi ya rais na idara ya mahakama?
Pia majaji wataamua ikiwa uhuru wa majaji umeingiliwa na DPP?
Akipeleka faili hiyo kwa CJ kuteuliwa kwa majaji watakaosikiza kesi ya DCJ Mwilu na DPP, Jaji Enock Chacha Mwita , alisema, “Kesi hii hii inaimbua maswali magumu na nyeti ya kikatiba yanayofaa kusikizwa na kuamuliwa na jaji zaidi ya mmoja.”
Jaji Mwita aliyekuwa ameombwa na DCJ Mwilu kupitia kwa mawakili wake aamue kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa na jaji mmoja , alisema “mtazamo wa majaji zaidi ya mmoja hauwezi lingana na wa mmoja.”
Alikubaliana na DPP kuwa kesi ya DCJ Mwilu iko na umuhimu wa kitaifa na ambao utaimarisha ustawishaji wa idara ya mahakama.
Kabla ya kuamuliwa kwa masuala haya , Jaji Mwita aliamuru DCJ Mwilu asifikishwe kortini kujibu mashtaka ambayo DPP alimfungulia.