ODM yapanga kumvua Obado ugavana
Na Elisha Otieno
MASAIBU yanazidi kumkumba Gavana Okoth Obado, baada ya ODM kuanzisha kampeni ya kuwataka madiwani wa Kaunti ya Migori kupiga kura ya kumwondoa uongozini.
Mwenyekiti wa chama hicho Kaunti ya Migori, Bw Philip Makabong’o anasema kuna majadiliano ili ikiwezekana, Bw Obado aondolewe ofisini.
“Madiwani wana siku 14 kumwondoa gavana huyo, la sivyo chama kichukue jukumu hilo. Kwa hakika ODM tuko katika makini kuhusu jambo hili,” aliwambia wanahabari.
Bw Makabong’o alisema ODM kina mbinu kadhaa kitakazotumia kutekeleza jambo hilo, kwa kuwa kinaamini kuwa gavana ameshindwa kufikia matakwa ya maadili ya uongozi.
“Tuna madiwani zaidi ya 40 wa ODM kati ya madiwani wote 57. Mbali na kesi ya uhalifu inayomkabili mahakamani, Bw Obado si mwaminifu kwa uongozi wa chama,” akasema.
Gavana huyo atarejeshwa kortini Jumatano wiki hii kujua kama atapewa dhamana kuhusiana kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.