Habari MsetoSiasa

Waliosafiri Mecca walia juhudi zao za kumshukuru Sonko kuhujumiwa

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

KUNDI la Waislamu waliofadhiliwa na Gavana wa Nairobi Mike Sonko kusafiri mjini Mecca, Saudi Arabia sasa wanalia kwamba juhudi zao kumwona gavana huyo kumpa shukrani zimekuwa zikizuiwa na watu wachache waliohusika na safari hizo.

Mahujaji hao wanadai kwamba ajenti aliyehusika na mchakato mzima wa safari hiyo na mpiga picha wa kibinafsi wa gavana wamekuwa wakiwazuia kumwona baada ya malalamishi kuzuka kuhusu ufisadi na ufujaji wa ufadhili wa Sh3 milioni zilizotolewa kugharimia ibada zao.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali, makundi hayo yalisimulia jinsi yalivyozongwa na matatizo chungu nzima ikiwemo kulala njaa kwa siku tatu, kukosa mahema ya kulala na kutegemea misaada ya rubaa za mahujaji kutoka mataifa mengine baada ya ajenti wao kuwakimbia na kuwatelekeza.

“Tulipitia mtihani mkubwa wakati wa Hajj ambayo ilifadhiliwa na gavana wetu, Sonko. Licha ya hayo tumekuwa tukijaribu mara kadhaa kumwona na kumshukuru lakini baadhi ya waliohusika na safari hiyo wamekuwa kizingiti kwa sababu wanajua tutamweleza ukweli kuhusu matatizo na kufujwa kwa fedha alizotoa,” ikasema kundi hilo.

Wakiwa wamejawa na huzuni na masikitiko, kundi hilo lilishangaa zilizokoenda Sh2 milioni alizotuma Bw Sonko wakiwa Saudi Arabia ili kuwasaidia kujikimu baada ya habari kuchipuka kwamba walikuwa wakiteseka na kuomba misaada kutokana na fedha za awali kutotosha kugharamia kujikimu kwao.

“Kwa kweli msaidizi wa gavana alitueleza tukiwa Hajj kwamba Bw Sonko alituma Sh2 milioni na hata akaamrisha tuende tutoe hela hizo ila tulipokuwa njiani aligeuka na kuwa mkali sana akisema hakukuwa na haja ya kutoa pesa hizo ilhali Hajj ilikuwa ikielekea kukamilika. Alidai kwamba zingerejea kwa gavana baada ya siku chache,” ikasema kundi hilo.

Hata hivyo, ajenti aliyewasimamia Prof Hassan Kinyua ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Nairobi alikanusha madai ya kundi hilo akisema hakuna fedha zilizoliwa. Aliongeza kwamba mahujaji hao hawakuelewa kiwango cha ufadhili aliotoa gavana.

“Sh3 milioni za kwanza hazikugharimia vyakula, malazi, mnyama wa kuchinja, usafiri wa teksi na pesa za matumizi. Fedha alizotuma baadaye ambazo niliambiwa ni Sh2 milioni hazikuweza kutolewa kwa sababu mpigapicha wake/msaidizi hakuwa na pasipoti na zilirejea kwa gavana,” akasema Bw Kinyua.

Aidha, akizungumza na Taifa Leo msaidizi wa gavana Farhan Abdulfata Ibrahim alikataa kutoa ufafanuzi wa kuridhisha akisema pesa zilirejea kwa gavana na haelewi kwa nini kundi hilo lipiganie kuonana naye ilhali walimfikishia shukrani na zawadi kutoka Mecca kwa niaba yao.

Juhudi za kumfikia Bw Sonko kuthibitisha kwamba pesa zilirejeshwa katika akaunti yake hazikufua dafu kwa kuwa hakupokea simu au kujibu ujumbe wetu. Hata hivyo, kundi hilo linashangaa iweje alitoa ufadhili nusu na kuwasababishia mahangaiko bila kuwajuza kabla hawajawajibikia ibada hiyo.

“Lau tungejua kwamba hali ingekuwa kinyume basi hatungeenda ila ilikuwa mtihani kwetu na tunaomba mola akubali dua zetu. Hata hivyo lazima tufahamu ukweli wa mambo ili kuwaepusha wenzetu kupitia madhila kama yetu,” wakaongeza kundi hilo.