• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
24 wanaswa katika msako dhidi ya Mungiki

24 wanaswa katika msako dhidi ya Mungiki

Na NICHOLAS KOMU

WATU 24 walikamatwa katika Kaunti ya Nyeri kwa kuhusishwa na kundi haramu la Mungiki, huku wahalifu wawili sugu waliokuwa wakisakwa wakijisalimisha kwa polisi.

Watu hao walikamatwa wikendi kwenye msako dhidi ya kundi hilo linaloibuka upya katika eneo la Kati.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nyeri, Bw Ali Nuni, alisema wengi wao ni vijana wenye umri wa miaka ya ishirini na walikamatwa katika maficho yao mjini Nyeri wakazuiliwa katika kituo cha polisi mjini humo.

“Kwa sasa tunawahoji. Hatuwezi kuhatarisha usalama wa wakazi wa Nyeri na hatutalegeza kamba hadi tuwakamate wote,” akasema Bw Nuno.

Msako huo ulifikisha idadi ya watu waliokamatwa kwa kuhusishwa na Mungiki kuwa 115 katika eneo hilo.

Ripoti kutoka kwa kamati ya usalama katika eneo hilo inaonyesha kuwa washukiwa 80 walikamatwa Kiambu na wengine 11 wakapatikana Kaunti ya Nyandarua.

Huku hayo yakijiri, wahalifu wawili sugu katika Kaunti ya Nyeri ambao walikuwa wakitafutwa na polisi walijisalimisha katika makao makuu ya idara ya upelelezi wa jinai eneo hilo, baada ya msako wa miezi mitatu ulioshindwa kuwanasa.

Polisi wamekuwa wakiwatafuta Joseph Kang’ethe almaarufu kama Wakinanyu, na John Githinji anayefahamika pia kama Mrefu, kwa kuhusishwa na wizi wa kimabavu na pia kuhusishwa na kundi la Mungiki.

Wawili hao walijisalimisha kupitia kwa kikundi cha kutetea haki za binadamu cha Informaction na kile cha Muslim for Human Rights (MUHURI) wakidai maisha yao yamo hatarini.

Walidai polisi wamekuwa wakitaka kuwaangamiza tangu Julai baada ya mauaji ya aliyekuwa Chifu wa Lokesheni ya Kamakwa, Bw Kimiti Nyuguto.

You can share this post!

Washukiwa motoni kwa kuchafua kuta za seli kwa kinyesi ili...

Mudavadi na Weta watakiwa kuingia serikalini

adminleo