• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
TAHARIRI: Tusiachie wahuni wawajuhumu raia

TAHARIRI: Tusiachie wahuni wawajuhumu raia

NA MHARIRI

MAPIGANO ambayo yamezuka katika maeneo ya Kapedo kaunti ya Baringo na Marsabit yanafaa kuchunguzwa kwa kina.

Mizozo inayoendelea katika kaunti hizo mbili, mbali na kusababisha maafa, imejiri wakati ambapo watahiniwa wa mitihani ya kitaifa ya kidato cha Nne (KCSE) wanaanza. Wenzao wa darasa la nane wanatarajiwa kufanya mtihani huo wiki ijayo.

Ingawa sababu ni tofauti katika kaunti hizo mbili, cha msingi ni kuwa athari za mapigano hayo ni zile zile. Wanafunzi katika shule za maeneo husika wamekuwa wakijiandaa kwa mitihani kwa miaka kadhaa na sasa ni wakati wa kuvuna matunda ya juhudi zao.

Kuzua ghasia na mauaji sio tu kunawanyima watahiniwa nafasi ya kudurusu vyema waliyofunzwa, bali pia kunawafanya wapoteze matumaini ya kuwa na ufanisi wa aina yoyoyte.

Kwa bahati mbaya, mapigano hayo yakichunguzwa kwa makini, itabainika kuwa ama yanafadhiliwa na watu wenye ushawishi, au yanachochewa na wahalifu ambao nia yao si njema kwa jamii pana katika kaunti hizo mbili.

Jana idara ya upelelezi wa Jinai (DCI) iliwahoji wanasiasa kadhaa kuhusiana na mapigano hayo, ambayo yamesababisha mahangaiko na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Ingawa matokeo ya uchunguzi huo yanafaa kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ili apendekeze mashtaka, yanafaa kushughulikiwa kwa haraka hata kabla ya kwenda kortini, ili kuokoa mambo.

Imebainika kuwa shule 16 zimeshafungwa Marsabit na hali ni sawa na hiyo Kapedo, ambapo wanafunzi wanahangaika wakitafutiwa sehemu salama za kwenda kufanyia mitihani yao.

Nchi hii ina idara kamili inayosimamia usalama wa ndani. Ni idara iliyopewa mamlaka yote na wananchi kupitia katiba, ili kuhakikisha kwamba maisha na shughuli za wananchi zinaendelea bila ya kuvurugwa na vitendo vya uhalifu.

Elimu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika maisha ya sasa. Iwapo watu watawanyima watoto wao kupata fursa ya kufanya mitihani, eti kwa sababu wanasiasa wachache wanataka kutimiza malengo ya kibinafsi, basi tutakuwa tumefeli.

Wadau wote wanapaswa kushirikiana na kuwakomboa wanafunzi pamoja na wanawake na watoto kutoka kwa ukorofi wa wahuni, wanaotumia nafasi za uongozi kuendeleza machafuko.

You can share this post!

Simba Coach taabani kwa kunaswa ikisafirisha mifuko 8.5...

Ajabu kampuni maarufu ya sigara kutaka wateja waache uvutaji

adminleo