WANDERI: Tuepuke dhana ya kipebari kwenye vitabu vya watoto wetu
Na WANDERI KAMAU
MOJAWAPO wa kurasa kwenye kitabu cha shule ya msingi unaonyesha mbunge fulani akiwasili kwa helikopta shuleni huku akishangiliwa na wanafunzi na kupokelewa kwa taadhima.
Na kama ilivyo, ulikemewa na wengi wakisema unasawiri uozo wa mtazamo wetu wa siasa na jamii kwa suala zima la kujilimbikizia mali.
Katika ukurasa huo tata, wanafunzi wanamsifia mbunge wao “kwa kufika shuleni akiwa amevalia vipuli na mavazi ghali.”
Cha kutia moyo ni kwamba, kwa kauli moja Wakenya waliungana kukosoa kitabu hicho, wakikitaja kuwa “hatari kwa mustakabali wa wanafunzi wachanga, hasa katika ufahamu wa msingi wa falsafa za kisiasa za nchi.”
Vile vile, ni tukio lililokifanya Chama cha Wachapishaji Kenya (KPA) kujitokeza wazi kujitetea kwamba wanachama wake hawakuhusika kwa vyovyote vile katika uchapishaji wa vitabu hivyo.
Katika majibizano hayo, kile kiliibuka wazi ni jinsi tulivyotaasisisha dhana za kibepari kama dira kuu ya siasa zetu. Je, makosa hayo yaliibuka kimakusudi bila ufahamu wa waandishi wa vitabu hivyo?
Lengo kuu lilikuwa lipi, ikizingatiwa kuwa mfumo wa sasa unajikita katika usisitizaji wa maadili miongoni mwa wanafunzi? Kilicho wazi ni kwamba, siasa zetu ni za kibepari; mfumo hatari unaodunisha utu na kushadidia ubinafsi kama nguzo kuu ya uanadamu. Ubepari ni hatari, kwani huigeuza jamii kuwa sawa na ya mahayawani wasiojaliana hali hata kidogo.
Ni mfumo ambao huathiri akili ya mwanadamu hivi kwamba mmoja humwona mwenzake kama adui, badala ya rafiki aliye katika safari moja ya kimaisha.
Baada ya Kenya kujinyakulia uhuru 1963, hayati Mzee Jomo Kenyatta alianzisha mwito wa ‘Harambee’ kama msingi wa kushinikiza ushirikiano wa jamii katika masuala muhimu kama ya kielimu.
Maana ya awali ya mfumo huo ilikuwa kwa wanajamii kuinuana kusomesheana watoto, kulipa bili za hospitali, kujengeana makanisa na kuanzisha miradi ya kuifaa.Hata hivyo, hilo lilibadilika baada ya waanzilishi hao kuaasi maana halisi ya mfumo huo kwa kupora mali ya umma.
Kwa wakati mmoja, Mzee Kenyatta alieleza jinsi viongozi walikuwa wamejitajirisha kwa mali waliyonyakua kutoka kwa wananchi. Alimuuliza mwanasiasa mkongwe, Bildad Kaggia kuhusu kile alichokuwa amejinyakulia tangu aanze kuhudumu serikalini mnamo 1964.
Hilo bila shaka lilionyesha jinsi nafsi za viongozi zilivyobadilika pindi walipochukua mamlaka. Kwa sasa, kilichobaki kwa Wakenya ni kufufua upya maana halisi ya ‘Harambee’ kwa ustawi halisi wa kijamii.