Ufadhili wa mabilioni kujenga nyumba za bei nafuu
Na BERNARDINE MUTANU
Idara ya Ujenzi wa Nyumba imepokea Sh47.25 bilioni kukamilisha mpango wa kujenga nyumba za bei nafuu kwa wananchi katika ajenda ya maendeleo.
Hii ni baada ya Hazina ya Fedha kuandaa tena bajeti ya matumizi ya fedha kwa lengo la kufanikisha ajenda hiyo ya maendeleo.
Rais Uhuru Kenyatta alitia sahihi sheria ya bajeti ya fedha za matumizi Jumanne na kutoa idhini kwa Hazina ya Fedha kutoa Sh21 bilioni kutoka kwa hazina ya pamoja kuipa Idara ya Ujenzi ambayo inaongoza ujenzi wa nyumba ambazo wananchi wanaweza kumudu.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Baraza la Mawaziri kupitisha kanuni za nyumba ambazo wananchi wanaweza kumudu wiki jana.
Mpango wa nyumba ni moja ya sekta nne chini ya “Big 4 Agenda” mpango aliotumia kufanya kampeni kuchaguliwa kwa awamu yake ya pili itakayoisha 2022.
Katika taarifa, Ikulu ilisema Rais alitoa idhini ya kutolewa kwa Sh873 milioni kwa Idara ya Wanyamapori na Sh2 bilioni kwa lengo la kupigia debe utalii.
Wizara ya Ujenzi ilipata Sh1.9 bilioni na Idara ya Mahakama Sh 1.5 bilioni.