Habari MsetoSiasa

Obado sasa kulala nyumbani baada ya baridi ya siku 34 ndani ya seli

October 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA 

HATIMAYE Gavana wa Migori Okoth Obado sasa ni huru baada ya mawakili wake kufaulu kutimiza masharti yote ya dhamana aliyopewa Jumatano.

Aliondoka katika gereza la Industrial Area kwenda nyumbani kwake Alhamisi saa mbili za usiku baada ya kufungiwa huko kwa siku 34 tangu alipokamatwa kuhusiana na mauaji ya kinyama ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno.

Mnamo Jumatano Bw Obado alilala katika rumande hata baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Jessie Lessit kumwachilia kwa dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini wa kiasi kama hicho.

Hata hivyo, kulikuwa na hitalafu moja ya magari yake mawili ambayo alikuwa ametoa kama mdhamini. Magari hayo ni aina ya Toyota Prado na Toyota Land Cruiser V8 ya thamani ya Sh5 milioni kila moja. Kasoro hiyo haikuweza kusuluhishwa afisi za mahakama zilipofungwa.

Mnamo Jumatano Jaji Lessit alimpa Obada dhamana lakini kwa sharti kwamba hataruhusiwa kusafiri nje ya nchi.

Hakama hiyo pia ilimzuia kwenda karibu na eneo la mauaji kwenye mpaka wa Kaunti za Migori na Homa Bay. Hii ina maana kuwa atahitajika kutoenda popote hadi kesi yake itakaposikizwa tena.

“Na mahakama hii inaweza kufutilia mbali dhamana hii ikiwa mshtakiwa atakiuka masharti yake,” akasema Jaji Lessit.

Hata hivyo Mbw Michael Oyamo na Karani wa Kaunti ya Migori Caspal Obiero ambao wameshtakiwa pamoja na Bw Obado wataendelea kukaa rumande baada ya kunyimwa dhamana.

Hii, kulingana na mahakama, ni kwa sababu kuna ushahidi wa kuonyesha kuwa walihusika moja kwa moja na mauaji ya marehemu Sharon, kwani ilibainika kuwa walifika eneo la mauaji.