TAHARIRI: Ni aibu kwa waziri kutoheshimu hadhi
NA MHARIRI
VIONGOZI wa kidini Kaunti ya Kakamega wamechukua jukumu la kuwapatanisha Seneta wa kaunti hiyo Bw Cleopas Malala na Waziri wa Michezo Rashid Echesa, kutokana na uhasama ambao umekuwa kati yao.
Wawili hao wameonyesha hadharani kutoelewana kwao, ambapo wamefikia hata kuharibiana sifa mitandaoni.
Waziri Echesa inadaiwa aliwalipa wanahabari watatu kuunda picha bandia ya seneta Malala akiwa uchi, almradi akabiliane naye kisiasa.
Viongozi hao wawili wameonyesha kukosa uwajibikaji, ikizingatiwa kuwa ni vijana wanaopaswa kuonyesha wengine jinsi ya kuwa na uongozi mzuri. Wakenya wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwakataa viongozi vijana. Hata Rais Kenyatta wiki jana alilalama kuwa viongozi vijana hawajafanya maendeleo makubwa wakilinganishwa na wenzao wazee.
Rais Mstaafu Daniel Arap Moi alikuwa akisisitiza kuwa vijana ni viongozi wa kesho. Japokuwa kesho yao imeshafika, ni dhahiri kuwa vijana bado wana safari ndefu ya kufikia vigezo vya uongozi mzuri, hasa kutokana na vitendo vya wanasiasa hao wawili.
Ni aibu kwamba viongozi hao vijana wanapoteza mwelekeo kwa njia inayoweza kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao, kwa kuanika tofauti zao mbele ya umma.
Aidha, tabia hiyo ya viongozi hao ni kinyume na kanuni kuhusu Maadili na Uongozi. Katiba yetu katika Sura ya Sita, inaeleza wazi kwamba viongozi wanatarajiwa kuwa na sifa za aina gani. Mojawapo ya sifa hizo ni kwamba wawe watu wenye tabia njema kama watu binafsi.
Waziri Echesa anapaswa kufahamu zaidi kanuni hizo, kwa kuwa wadhifa wake sio tu unamuonyesha yeye kama mti binafsi, bali pia yule aliyemteua. Kwa kuendeleza tabia zinazodhihirisha uhuni, waziri anafanya wananchi na umma kwa jumla watilie shaka uteuzi wake.
Wadhifa wa uwaziri umebuniwa kwenye katiba ili apewe mtu ambaye atakuwa tayari kuwatumikia wananchi. Wajibu wa waziri ni kuunda sera zitakazowezesha serikali kutimiza mipango yake ya maendeleo.
Katiba ilipopendekeza kuwa mawaziri wasiwe miongoni mwa wanasiasa, ilikuwa ina dhamira ya kuhakikisha ni watu wenye nia ya kuchapa kazi pekee watakaoteuliwa kuhudumu. Kwa kuwa Rais aliona vyema kuwapa nafasi baadhi ya wanasiasa kuwa mawaziri, hawana budi kumpa heshima anayostahili kwa kuepuka siasa duni.