• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
Juhudi za kuwapatanisha Echesa na Malala zaanza

Juhudi za kuwapatanisha Echesa na Malala zaanza

Na SHABAN MAKOKHA

VIONGOZI wa kidini kutoka Kaunti ya Kakamega wamejitolea kupatanisha Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na Waziri wa Michezo Rashid Echesa kufuatia uhasama uliopo kati yao.

Wanachama wa baraza la viongozi wa kidini ambalo lina viongozi wa Kanisa Katoliki, Waislamu, Anglikana, Wahindu na makanisa mengine ya Pentekosti walisema wanatafuta viongozi hao wawili ili kuwapatanisha.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Askofu Nicholas Olumasai, aliomba wawili hao kukubali juhudi zinazoendelezwa na viongozi wa kidini.

“Ni uchungu kuona viongozi wetu vijana wakipoteza mwelekeo kwa njia inayoweza kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao baada ya kuanika tofauti zao mbele ya umma. Kama taasisi iliyo na jukumu la kupatanisha taifa, tumejitolea kupatanisha wawili hawa na kuhakikisha watakula pamoja,” akasema.

Bw Olumasai aliongeza kuwa baraza hilo limemtwika jukumu Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Kenya, Sheikh Abdalla Ateka, kumtafuta Bw Echesa ili azungumze naye kibinafsi kuhusu pendekezo hilo huku Katibu Mwandalizi wa baraza hilo, Askofu Johnston Wandera, akitumwa kuzungumza na Bw Malala.

Bw Wandera alimshauri Bw Malala na Bw Echesa wakubali hatua ya wazee wa jamii na viongozi wa kidini.

“Wawili hao wanaangaliwa kama mfano na vijana wengi Kakamega na kwingineko kitaifa na tunataka kuwafanya waongoze kampeni ya watu kuishi na wenzao kwa amani,” akasema.

Sheikh Ateka alisema ajenda kuu ni kuhakikisha wawili hao watashauriawa kupigania maslahi ya kitaifa badala ya kujitafutia makuu ya kibinafsi.

“Tunawataka wasameheane. Tunawataka watusikilize na wakubali wito wetu wa kuwapatanisha ili watu wengine wasitumie uhasama wao kuwatenganisha zaidi,” akasema Bw Ateka.

Wakizungumza kwingineko, wabunge Elsie Muhanda (Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kakamega) na Emmanuel Wangwe (Navakholo), waliomba viongozi hao wawili wakomeshe mizozo yao.

“Mivutano yao isiyokuwa na kikomo inazidi kusababisha wasiwasi katika kaunti hii. Hatua zao zinaenda kinyume na matarajio ya wafuasi wao,” akasema Bi Muhanda, wakati wa mazishi ya Bw Jacob Nanjakululu, ambaye alikuwa mwanachama wa Chama cha Amani National Congress. (ANC).

Kwa upande wake, Bw Wangwe alimtaka Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa azungumze na Bw Echesa na Bw Malala ili wakomeshe uhasama wao.

You can share this post!

Mtahiniwa wa KCSE aanguka na kufariki

MAHINDI TELE, UGALI GHALI

adminleo