MAHINDI TELE, UGALI GHALI
Mwangi Muiruri na Cecil Odongo
HOFU ya kushtakiwa kwa maafisa wanaoshukiwa kuhusika katika sakata ya mahindi ndicho kiini kikuu cha uhaba wa mahindi, ambao Jumatatu ulifanya wasagaji kutangaza wataongeza bei ya unga hadi Sh100 na zaidi.
Pia hatua ya wakuzaji mahindi eneo la North Rift kupinga makubaliano ya kuuza mahindi kwa bei nafuu imechangia uhaba huo.
Duru za kuaminika ndani ya Serikali zilieleza Taifa Leo kuwa kuna mashauriano yanayoendelea ya kutafuta uwezekano wa washukiwa kurudisha mahindi waliyonunua kwa njia zisizo halali kwa wafanyibiashara waliyouzia NCPB, ili nao wairudishie pesa ambazo walilipwa.
Hii ni kutokana na shinikizo ambazo Rais Uhuru Kenyatta amewekea Wizara ya Kilimo akiitaka kuhakikisha wakulima wamelipwa pesa zao haraka iwezekanavyo.
Ni kutokana na hali hii ambapo NCPB imesita kuuzia wasagaji mahindi kwa bei ya Sh1,600 kwa gunia la kilo 90 kama Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri alivyoahidi mwezi uliopita ili kuwawezesha wasagaji nao kuteremsha bei hadi Sh75.
Duru zilidokeza kuwa bodi hiyo inahisi kuwa iwapo itauza mahindi kwa Sh1,600 kama Bw Kiunjuri alivyokubaliana na wasagaji, kisha maafikiano ya kurudisha mahindi na pesa yafaulu, watapata hasara ikizingatiwa waliyanunua kwa Sh3,200 kutoka kwa wafanyibiashara waliyoyaagiza kutoka nje ya nchi na hivyo kupungukiwa na pesa wanazofaa kurudisha.
Sakata hiyo ilizuka mwishoni mwa mwaka jana NCPB iliponunua mahindi yaliyoagizwa kutoka nje ya nchi kwa pesa zilizokusudiwa kuwalipa wakulima wa humu nchini. Hatua hiyo imefanya bodi hiyo kupungukiwa na pesa za kulipa wakulima.
Hapo jana, Bw Kiunjuri aliambia Taifa Leo kuwa ahadi ya Serikali kuuza mahindi kwa wasagaji kwa Sh1,600 ingalipo akiongeza kuwa hifadhi ya mahindi nchini tayari ina mahindi ya kutosha.
Kwenye maafikiano na wasagaji unga kuhusu kupunguzwa kwa bei hadi Sh75 mwezi jana, Serikali iliahidi kuhakikisha imewauzia wasagaji mahindi yaliyo NCPB kwa bei nafuu ya Sh1,600 ili kuwawezesha nao kuteremsha bei ya unga.
Lakini ahadi hiyo imegeuka kuwa hewa baada ya wasagaji kusema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahindi sokoni. Hii inamaanisha kuwa Serikali haikuheshimu ahadi yake ya kuuza mahindi kwa bei nafuu ili kuwezesha wasagaji kuteremsha bei zao
Mwenyekiti wa muungano wa wasagaji, Bw Peter Kuguru, alisema hawana mahindi yoyote katika hifadhi zao.
“Bei ya unga itapanda hadi Sh100 na zaidi katika maeneo mbalimbali kuanzia mwishoni mwa wiki kwa sababu hatuna mahindi ya kusaga. Serikali inaonekana haina nia ya kupunguza uhaba huo kwa kutoa mahindi yanayohifadhiwa na NCPB,” akasema Bw Kuguru.
Alisema kuwa maagizo ya Bw Kiunjuri kuwa unga wa pakiti ya kilo mbili uuzwe kwa Sh75 hayawezi kutekelezeka ikiwa bei ya mahindi itaendelea kuwa ya juu.
“Inasikitisha kwamba tunapitia hali ngumu wakati ambapo mahindi yamejaa katika mabohari ya serikali. Pia hatuwezi kununua kutoka kwa wakulima kwa sababu wanauza kwa bei ya juu,” akaeleza Bw Kuguru.
Mkurugenzi wa Muungano wa Wakulima nchini Kipkorir Menjo alisema hatua ya kupendekeza mahindi kuuzwa kwa Sh1,600 kwa gunia haikujali maslahi ya wakulima.
“Hakuna mkulima anayeweza kukubali kuiuzia NCPB au kampuni za kusaga mahindi kwa sh1600 jinsi walivyokubalina kwa sababu hiyo ni hasara kubwa sana kwetu. Makubaliano hayo hayakuhusisha mkulima wala kuyazingatia maslahi yake,” akasema Bw Menjo.