KCPE yaendelea wasichana watatu wakijifungua
Na WAANDISHI WETU
MTIHANI wa mwaka huu wa darasa la nane (KCPE) ulianza Jumanne huku wasichana watatu wakiufanyia hospitalini baada ya kujifungua.
Wawili kati ya watahiniwa hao wanatoka Kaunti ya Homa Bay na mmoja Kaunti ya Kwale.
Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Bw Karuku Ngumo alisema msichana huyo alikimbizwa hospitali ya Kwale ambako alijifungua mtoto wa kiume.
“Msichana huyo alikimbizwa hospitalini baada ya kuhisi maumivu ya kujifungua kabla ya mtihani kuanza,” alisema Bw Karuku.
Nao watahiniwa wawili kutoka Kaunti ya Homa Bay walifanyia mtihani katika hospitali tofauti baada ya kujifungua. Mkurugenzi wa elimu wa kaunti hiyo Bi Margaret Mwandale alisema watahiniwa hao watafanyia karatasi zilizobaki za mitihani wakiwa hospitalini.
“Hawana nguvu na wanatatizika kutembea. Watafanyia mtihani wote hospitalini,” alisema afisa huyo na kuongeza kuwa maafisa wa polisi wanawake wametumwa kuwashughulikia wakifanya mtihani hospitalini.
Katika kisa kingine, mtahiniwa kutoka shule ya msingi ya Keringet, Kaunti ya Nakuru alilazwa katika hospitali ya Nakuru baada ya kuugua.
Mwanafunzi mwingine anafanyia mtihani katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi mjini Eldoret alipopelekwa kuwekwa figo.
Msichana mwingine katika shule ya msingi ya Iruri wilaya ya Maara, Kaunti ya Tharaka Nithi alishambuliwa kwa kisu akielekea shuleni na kijana anayedaiwa kuwa mpenzi wake.
Kulingana na polisi, msichana huyo alichomwa kisu kichwa mita machache kutoka shuleni.
OCPD wa Maara, Johnston Kabusia alisema msichana huyo alipewa huduma ya kwanza kabla ya kuruhusiwa kufanya mtihani wa hisabati.
“Msichana huyo alipewa msaada wa huduma ya kwanza na amejiunga na watahiniwa wengine ingawa ana maumivu,” Bw Kabusia alisema.
Mkuu wa elimu katika kaunti hio, Bi Ann Kiilu alisema kijana huyo alikuwa amemuonya asifanye mtihani akisema alitaka kumuoa.
Kwenye kisa kingine Nakuru, msimamizi wa mitihani eneo la Naivasha alifutwa kazi kwa kusafirisha karatasi za mtihani bila kuandamana na maafisa wa usalama.
Habari zilisema afisa huyo aliondoka kituo cha kusambaza karatasi za mitihani bila maafisa wa usalama kinyume cha kanuni za mitihani.
Katika kisa kingine Kaunti ya Kajiado, mlinzi alikamatwa akiwa na karatasi feki za mtihani.
Kaunti ya Migori, watahiniwa watatu walikosa kufanya mitihani baada ya shule yao kukosa kuwasajili kulingana na kanuni za Baraza la Mitihani (KNEC).
Katika gereza la Shimo la Tewa, Kaunti ya Mombasa, watahiniwa 11 wa kitengo cha kurekebishwa tabia za watoto, hawakufanya mtihani baada ya majina yao kukosekana katika sajili ya watahiniwa.
Ripoti za Eric Matara, George Sayagie, Macharia Mwangi, John Njoroge, Steve Njuguna. Benson Amadala, Magati Obebo, Elizabeth Ojina, Victor Raballa, Vitalis Kimutai, Derrick Luvega, Elisha Otieno, Fadhili Fredrick na Ahmed Mohammed