• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Gavana wa Lamu aapa kufurusha wafanyakazi wote hewa

Gavana wa Lamu aapa kufurusha wafanyakazi wote hewa

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kaunti ya Lamu imetangaza vita vikali dhidi ya wafanyikazi hewa eneo hilo.

Gavana wa Lamu, Fahim Twaha, anasema ili kukabiliana na tatizo la kuwepo kwa wafanyikazi hewa eneo hilo, serikali yake imesitisha utoaji wa kandarasi mpya au kuongeza muda zile ambazo muda wake wa kuhudumu umekwisha hadi pale utambuzi na uharamishaji wa wafanyikazi hewa utakapokamilika.

Akizungumza wakati alipozuru kwenye hospitali kuu ya King Fahad mjini Lamu Jumatano, Bw Twaha alikiri kuwepo kwa wafanyikazi ambao si halali na ambao wamekuwa wakipokea mishahara kutoka kwa kaunti bila kufanya kazi yoyote eneo hilo.

Alisema utawala wake tayari umezindua shughuli ya kuwasaka na kuwafuta wafanyikazi hewa kabla ya kufikiria kuajiri upya wafanyakazi wengine wanaohitajika.

Alisema shughuli ya kuwasaka wafanyikazi hewa inatekelezwa katika sekta zote za kaunti, ikiwemo ile ya afya, elimu, uhasibu miongoni mwa sekta zingine.

Aliwataka wale ambao muda wa kuhudumu kwa kandarasi zao umeisha na wanahitaji kuandikwa upya kusubiri zoezi la kuwatafuta wafanyikazi hewa kukamilika kufikia mwezi Novemba mwaka huu.

 “Kaunti haitaongeza muda wa kandarasi za wafanyikazi hadi pale tutakapokamilisha shughuli ya kuwatafuta na kuwafuta wafanyikazi hewa. Tatizo hilo limekuwepo kwa mud mrefu hapa Lamu na tunataka kulimaliza. Shughuli ya ukaguzi wa wafanyikazi hewa inatekelezwa katika sekta zote na tutafikiria kuongeza muda wa kandarasi kwa wafanyikazi wetu punde zoezi hilo litakapokamilika kufikia Novemba mwaka huu,” akasema Bw Twaha.

Aidha aliwatahadharisha wafanyikazi wote wa kaunti dhidi ya kujihusisha na ufisadi.

Alisema utawala wake uko macho na kwamba atahakikisha wale watakaopatikana wakijihusisha na ufisadi wanafutwa kazi na kushtakiwa.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Idara ya Afya Kaunti ya Lamu, Abubakar Badawy alisifu juhudi zinazotekelezwa na kaunti ya Lamu katika kuhakikisha sekta ya afya inaboreshwa zaidi eneo hilo.

Bw Badawy aliahidi kwamba wafanyakazi katika idara yake watatekeleza kila juhudi ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Lamu.

You can share this post!

Mama Jowie azirai kortini baada ya kilio mwanawe...

DPP na EACC wazimwa kumshtaki Gavana Mutua kwa sakata ya...

adminleo