DPP na EACC wazimwa kumshtaki Gavana Mutua kwa sakata ya magari
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya rufaa Jumatano ilitimatatisha kesi ya ufisadi dhidi ya Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua iliyotokana na ununuzi wa magari 16 pasi kufuata sheria na yaliyogharimu ma milioni ya pesa.
Majaji Roselyn Nambuye, Asike Makhandia na James Otieno Odek walisitisha hatua ya kumfungulia Gavana Mutua mashtaka kutokana na ununuzi wa magari hayo
“Hii mahakama imezima hatua ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) na tume ya kupambana na ufisadi (EACC) ya kumshtaki Dkt Mutua kwa ununuzi wa magari hayo kinyume cha sheria za ununuzi,” walisema majaji Nambuye, Makhandia na Odek.
Majaji hao walitoa agizo hilo kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya mawakili wa DPP, EACC na Wilfred Nyamu.
Katika makubaliano yaliyowasilishwa mahakamani DPP na EACC waliihakikishia mahakama kuwa hawatamfungulia mashtaka Dkt Mutua kwa ununuzi wa magari hayo yanayotumika kama ambulansi na magari ya kushika doria.
Bw Nyamu aliambia mahakama kuwa Dkt Mutua aliokoa pesa za umma kwa kununua magari kuu kuu na masalio ya pesa hizo zaidi ya Sh51 milioni akatumia kuweka barabara lami katika kaunti hiyo.
Tume ya EACC ilikuwa imepewa kibali cha kumshtaki Dkt Mutua na aliyekuwa Jaji wa Mahakama kuu sasa Jaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola.
Mahakama ilifahamishwa na Bw Nyamu kuwa kesi dhidi ya Dkt Mutua ilikuwa iunganishwe na nyingine iliyokuwa imewasilishwa dhidi ya mawaziri waliohusika na ununuzi huo wa magari walioachiliwa Novemba 17, 2017 na hakimu mkazi Mahakama ya Machakos.
Katika ombi lake la kupinga akishtakiwa Dkt Mutua alisema kuwa hakuwa afisa muhusika na ununuzi wa bidhaa katika kaunti hiyo.
Alisema idhini ya ununuzi wa magari hayo ilitolewa na mamlaka ya uzinduzi wa serikali za kaunti (TA).
Alijitetea kuwa hajui sababu ya kuandamwa ashtakiwe na aliokoa mamilioni ya pesa za umma katika ununuzi wa magari yasiyo mapya kwa mawaziri wake.
Aliongeza kusema kuwa kamati ya kaunti inayohusika ilipitisha mwaka wa 2013 magari hayo yanunuliwe. Aliyekuwa seneta wa Machakos Johnstone Muthama aliandikisha madai kwa EACC akidai pesa za umma zimefujwa na Dkt Mutua.